Habari Mseto

COVID-19: Mhadhiri wa UoN afariki

August 1st, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MHADHIRI mtajika wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) Ken Ouko amefariki kutokana na changamoto za kiafya zilizosababishwa na virusi vya corona.

Mkurugenzi wa mawasiliano katika chuo hicho John Orindi, amethibitisha Jumamosi asubuhi kuwa Dkt Ouko alifariki katika Hospitali ya Aga Khan ambako alikuwa amelazwa akipokea matibabu.

Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi Profesa Stephen Kiama ametaja kifo cha mhadhiri huyo wa taalamu ya Soshiolojia kama hasara kubwa kwa chuo hicho.

Kiama alisema kufikia Jumamosi chuo hicho kimepoteza wafanyakazi wanne kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

“Ni hasara kubwa kukuza wataalamu wa kutegemewa kisha wanafariki wakati ambapo huduma zao zinahitajika zaidi,” Naibu Chansela huyo akasema kwenye taarifa.

Marafiki wa karibu wa Dkt Ken wamemuomboleza kupitia risala walizozituma kupitia mitandao ya kijamii.

“Ni huzuni kuu kupokea habari za kifo cha ndugu yangu mkubwa Dkt Ken Ouko. Makiwa kwa familia,” William Odek akaandika katika Facebook.

“Dkt Ken Ouko alikuwa mhadhiri shupavu. Alifanya taaluma za Saikolojia na Soshiolojia kuwa rahisi na nyepesi. Ni huzuni kuwa Covid-19 imekatiza maisha yake,” Afisa wa ODM/NASA Norman Magaya akasema kupitia Twitter.

Marehemu alikuwa maarufu katika vipindi vya runinga ambapo alitoa ushauri kuhusu masuala kadhaa ya kifamilia.

Mnamo Ijumaa, watu 16 zaidi walithibitishwa kufariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 Ijumaa huku visa 732 vipya vya maambukizi vikiripotiwa, Wizara ya Afya ilisema.

Vifo vya wagonjwa hao sasa vimefikisha 341, idadi jumla ya wale ambao wamefariki kutokana na ugonjwa huo nchini Kenya kufikia Ijumaa, Julai 31, 2020.

Na idadi jumla ya walioambukizwa tangu virusi vya corona vithibitishwe kwa mara ya kwanza nchini imevuka kima cha 20,000 na kufikisha watu 20,636.

Visa 723 vipya vilipatikana baada ya watu 8,679 ambao sampuli zao zilifanyiwa uchunguzi ndani ya kipindi cha saa 24 kuanzia Alhamisi. Kwa hivyo, kufikia Ijumaa jumla ya sampuli 303,959 zimepimwa nchini tangu kisa cha kwanza cha maambukizi ya corona kitangazwe nchini mnamo Machi 13, 2020.

Akihutubia wanahabari katika makao makuu ya Wizara ya Afya Nairobi Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisem wagonjwa wengine 44 walipona na hivyo kufikisha idadi jumla ya waliopona kuwa 8,165.

Wagonjwa 24 miongoni mwa waliopona ni wale ambao wamekuwa wakiuguzwa nyumbani huku wengine 20 walikuwa wakitibiwa katika hospitali mbalimbali.

Kwa mara nyingine Nairobi inaendelea kuandisha idadi kuwa visa vipya vya maambukizi ambayo ilikuwa 436, ikifuatwa na kaunti ya Nakuru yenye visa 83, Mombasa (43) na Kiambu (45).

Visa vingine vipya viligunduliwa katika kaunti zingine kama ifuatavyo: Turkana (12), Uasin Gishu (10) Machakos 9, Kajiado (9), Busia (8), Muranga (7), Kericho(7) , Kisumu (6), Baringo (5),Bomet (5), Garissa (3), Kwale (3), Nyeri (3) na  Siaya (3),

Kaunti za  Isiolo ,Kakamega, Lamu, Meru, Wajir, Taita Taveta, Tana River na  Vihiga ziliandikisha visa viwili kila moja huku  Nyandarua, Elgeiyo Marakwet, Makueni, Marsabit na Kilifi zikirekodi kisa kimoja kila moja.

Waziri Kagwe alisema inasikitisha kuwa watu wenye umri mdogo wanaendelea kufariki kutoka na Covid-19 miongoni mwao wakiwa wale ambao hawajaathirika na magonjwa sugu awali.

“Tuna hofu kwamba kati ya vifo 30 vilivyoripotiwa ndani ya siku tatu, wengi wa watu hao ni watu wenye umri mdogo,” akaeleza.

Kwa hivyo Bw Kagwe alionya vijana kuondoa dhana kuwa hawako katika hatari ya kuangamizwa na Covid-19 ikilinganisha na watu wenye umri mkubwa.

“Kwa mfano, mwanamke mwenye umri wa miaka 22 alifariki katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH),” Bw Kagwe akasema, akiongeza kuwa wengine wanne wenye umri wa chini ya miaka 33 pia walifariki katika hospitali zingine.