Makala

COVID-19: Msichana, 12, amtungia mama ambaye ni muuguzi shairi kumpongeza kwa kazi nzuri

May 18th, 2020 2 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

MWANAFUNZI Ida Kibet, 12, alizoea kumkaribisha mamake nyumbani kwa kumkumbatia akitoka kazini, lakini janga la Covid-19 limesababisha mambo kubadilika.

Utaratibu huo wa awali ulimpa raha Ida kwani alifurahia sana kumuona mamake akitabasamu baada ya kazi nyingi hospitalini ambako anafanya kazi kama muuguzi.

Hata hivyo, hali hiyo ilikatizwa ghafla Machi 13, 2020, wakati kisa cha kwanza cha mgonjwa wa Covid-19 kilipotangazwa humu nchini na serikali.

“Habari za kwanza kabisa kuhusu kuthibitishwa kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini zilikuwa za kutamausha. Kukafuatia kanuni na masharti mengi kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta na Wizara ya Afya ambapo ‘tulizimwa’ kutangamana moja kwa moja na wapendwa wetu,” anasema Ida.

Licha ya kuwa kanuni hizo zilinuia kuzuia maambukizi zaidi , Ida ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya Little Lambs mjini Eldoret anasema kukosa kumkumbatia mamake kumemsababishia huzuni mwingi.

“Nililazimika kutunga na kuliandika shairi kuhusu corona ili kumpasha mama ujumbe niliokuwa nao moyoni. Ni mama mwenye bidii na amezidi kujikakamua kuona kuwa familia pamoja na wagonjwa hospitalini wanashughulikiwa bila ubaguzi,” anaeleza.

Kwenye shairi lake, Ida anazungumzia jinsi ambavyo ugonjwa wa Covid-19 umebadili hali ya maisha.

Baadhi ya mabadiliko ni wanafunzi kukosa kwenda shuleni, michezo mbalimbali kusitishwa, kukosa kucheza na watoto wenzake, kukosa kusalimiana na wazazi kila wanapotoka kazini, kuosha au kunawa mikono kila mara na kukaa nyumbani muda mwingi.

Hayo tu ni baadhi ya mambo aliyoyapa kipaumbele kwenye shairi hilo.

Anamsifia mamake kwa kazi nzuri na kumtaka awe makini zaidi wakati yuko kazini kwa sababu familia yake bado inamhitaji zaidi.

“Licha ya kuwa hakuna kukumbatiana tena kila mara unapofika nyumbani baada ya kazi, jua kwamba tunakuthamini na kukupenda sana. Kuwa makini kazini na kujikinga vilivyo na maambukizi kila wakati. Siku moja Corona itazama,” ni sehemu tu ya ujumbe uliomo kwenye shairi la Ida kwa mamake.

Ida ambaye ni kifungua mimba katika familia yao ya watoto watatu, anasema wakati huu anawatunza nduguze – kaka na dada – ambao ni pacha.

“Kwa sababu siku zote niko nyumbani na siwezi kwenda kucheza na watoto wengine kule nje, nimejifunza kuwachunga ndugu na dada yangu kwa kuhakikisha kuwa wanakula kwa wakati unaofaa na pia kuwafunza jinsi ya kukaa wakiwa wasafi,” anasema.

 

Mwanafunzi Ida Kibet, 12, wa Shule ya Msingi ya Little Lambs mjini Eldoret. Ametunga shairi kuhusu ugonjwa wa Covid-19 akimsifu na kumtia moyo mama yake ambaye ni muuguzi katika hospitali moja mjini humo. Picha/ Phyllis Musasia

Kulingana naye, anapomuona mamake akirejea nyumbani kila jioni na kisha kutoa nguo na kuoga kule nje kabla ya kuingia kwenye nyumba si jambo rahisi.

“Niligundua kuwa mama anahitaji sio tu kupigiwa makofi kwa bidii aliyonayo ila maneno mazuri ya kumpa nguvu na tabasamu wakati huu usiokuwa wa kawaida,” akasema huku akiongeza kuwa shairi lilimfaa zaidi.

Aidha, shairi hilo linawahimiza wananchi wote kuwa waangalifu na kufuata kanuni zote zilizowekwa ili kuwa salama.

Ida anawasihii wazazi wote kuwa waangalifu wakati wanapokuwa kazini na sehemu nyinginezo kama vile kwenye maduka ya jumla na soko huru, ili kuwaondolea wanao wasiwasi kuwa huenda wakaambukizwa virusi hatari vya corona.

Shairi lake linawashauri pia watoto kujizuia na michezo ya kiholela ambayo inahusisha makundi makubwa na badala yake kukaa manyumbani na kuhakikisha wanaosha mikono yao kila wakati na sabuni na maji mengi.

Shuleni, Ida anapendelea sana masomo ya Sayansi na Dini na angependa kuwa rubani mara awapo mkubwa.

Anapenda pia michezo ya kuigiza na nyimbo.