Makala

COVID-19: Muuguzi Sarah Mosop yuko mstari wa mbele kuwashughulikia wagonjwa

May 13th, 2020 3 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

[email protected]

KISA cha kwanza cha mgonjwa wa Covid-19 kilipotangazwa nchini Machi 13, 2020, muuguzi Sarah Mosop wa hospitali ya Nakuru alijua hali ingebadilika nchini ikiwemo mkondo wa maisha.

Tayari mambo yalikuwa mabaya katika mataifa yaliyopiga hatua kimaendeleo kama vile Italia, Uhispania, Marekani miongoni nchi nyinginezo.

Kulingana naye, Kenya haikuwa tofauti na mataifa hayo na alihofia mambo kuwa mabaya hata zaidi kufuatia kwa sababu wakati huo matayarisho yaliyokuwa yamefanywa hayakuwa ya kujitosheleza na kuridhisha katika kukabili maradhi hayo.

Visa vya maambukizi na idadi kubwa ya vifo vilizidi kuripotiwa kote duniani huku maelefu ya raia wa kawaida, viongozi pamoja na wahudumu wa afya wakiambukizwa na wengine kupoteza maisha yao.

“Covid-19 si ugonjwa wa kawaida kama vile malaria au homa ya matumbo. Kuthibitishwa kwa kisa cha kwanza nchini kulinitia tumbojoto kwani nilijua kulikuwa na mambo mengi ambayo yalistahili kurekebishwa na pia kupigwa jeki hasa katika sekta ya afya,” akasema Bi Mosop wakati wa mahojiano na Taifa Leo.

Hata ingawa wahudumu wa afya walikuwa tayari wamepewa mafunzo kuhusu jinsi ya kuwashughulikia wagonjwa na wale wanaoshukiwa kuwa na virusi vya corona, Bi Mosop anasema hofu ya kuambukizwa Covid-19 ilizidi kumjaa yeye pamoja na wahudumu wengine.

 

Muuguzi Sarah Mosop (kulia) katika hospitali ya Nakuru yuko katika mstari wa mbele kupambana na janga la Covid-19 nchini. Aelezea kuhusu safari yake kuwashughulia wagonjwa walioambukizwa. Picha/ Cheboite Kigen

Siku chache baadaye, wagonjwa walioambukizwa walianza kufika katika hospitali mbalimbali kwa matibabu.

Lakini kabla ya hayo, Bi Mosop anasema timu ya madaktari na wauguzi 25 iliteuliwa katika hospitali yao na kupewa mafunzo dhahiri jinsi ya kuwashughulikiwa wagonjwa wa virusi vya corona.

Bila kutarajia, Bi Mosop alichaguliwa kiongozi wa timu hiyo na hapo ndipo alianza kujitayarisha kwa kazi iliyokuwa inamsubiri.

“Tuliitwa katika mkutano na usimamizi wa hospitali hii na wakati wa uteuzi, madaktari na wauguzi walichaguliwa bila kuwepo kwa utaratibu wowote na hapo ndipo nilitangazwa kiongozi wa timu hiyo,” anasema Bi Mosop.

Kulingana naye, hakukuwepo nafasi ya kukataa majukumu mapya aliyopewa wala kutoa malalamiko.

“Kuanzia wakati huo, hali ilibadilika kabisa na ikawa tofauti sana na jinsi ambavyo tumezoea kuwashughulikia wagonjwa wa kawaida. Tulihitajika tuwe makini zaidi na jinsi ambayo tunapaswa kuwashughulikia wagonjwa wa Covid-19 ili kujikinga na kuwakinga wahudumu wengine dhidi ya maambukizi,” anasema.

Muuguzi Sarah Mosop katika hospitali ya Nakuru yuko katika mstari wa mbele kupambana na janga la Covid-19 nchini. Aelezea kuhusu safari yake kuwashughulia wagonjwa walioambukizwa. Picha/ Cheboite Kigen

 

Muuguzi huyu mwenye tajriba ya takriban miaka 25 anasema timu hiyo ilipata wakati mgumu majuma mawili ya mwanzo kwa sababu hospitali haikuwa na vifaa vya kutosha vya kujikinga kuepuka maambukizi.

“Tulikuwa na wagonjwa ambao walikuwa wametengwa kwa kuhofia kuwa walikuwa wameambukizwa ugonjwa huo lakini hospitali haikuwa na vifaa vya kutosha vya kujikinga na maambukizi. Vifaa kama vile barakoa, glavu na mavazi mengine yalikuwa hayatoshi,” anaeleza.

Changamoto hiyo ilizidi kushuhudiwa huku baadhi ya wahudumu wakitishia kususia majukumu ikiwa hali hiyo ingeendelea.

“Ilinibidi kujitwika majukumu zaidi na kuhakikisha wagonjwa wote wanapata huduma nzuri bila ubaguzi wowote. Kama kiongozi, nikijitolea kufanya kila niwezalo ili wagonjwa wapate vyakula, dawa za kupunguza maumivu na vifaa vingine walivyohitaji kwa matumizi yao ya binafsi,” anaeleza.

Hata hivyo, hali ilizidi kubadilika hata zaidi baada ya wagonjwa wa kwanza wawili kupatikana na virusi hivyo katika hospitali ya Nakuru.

Bi Mosop anasema changamoto zilizidi na ikafikia hatua ya kunyanyapaliwa hata na wafanyakazi wenzake, jamaa na marafiki.

“Kila aliyejua kwamba ninafanya kazi hospitalini, alijitenga nami na ikawa vigumu hata kutangamana na familia yangu nyumbani,” akasema.

Mwanawe mmoja alihama nyumbani na kwenda kuishi na jamaa zao kwa hofu kuwa huenda Bi Mosop akamwambukiza ugonjwa.

“Nilijihisi tofauti sana na asiye na maana licha ya bidii niliyokuwa nayo kuhakikisha wagonjwa wako sawa. Maombi ndiyo yameniweka hadi wakati huu,” anasema.

Bi Mosop anasema ilimbidi ajikakamue bila kuonyesha yale aliokuwa anapitia ili wagonjwa wapate nafuu haraka.

Wakawa kila wanapomuona wanatabasamu kwa imani kuwa hali yao itaimarika haraka.

“Wakati mwingi niliwazungumzia wagonjwa kuhusu umuhimu wa kuwa na imani ya kutosha kwa Mwenyezi Mungu. Nilisimama nje kwenye dirisha ili kupasha ujumbe na kuzungumza nao kwa manufaa yao na yangu mwenyewe kujikinga dhidi ya maambukizi,” anaongeza.

Baada ya wiki mbili, vipimo vilifanywa kwa wagonjwa hao na matokeo yakaonyesha kuwa bado walikuwa na virusi vya corona.

Bi Mosop anasema walivunjwa moyo na matokeo hayo ikizingatiwa bidii yao kuona kuwa hali ya wagonjwa inaimarika.

“Ilitubidi turudi kwenye kikao na kuzungumza kuhusu ni wapi tulienda vibaya. Tuliweka mikakati na kila mmoja akajizatiti kuona kuwa matokeo ya pili yatakapofanywa, yatakuwa mazuri,” anasema.

Muda uliyoyoma na baadaye sampuli nyingine zilichukuliwa kutoka kwa wagonjwa hao ambapo walithibitishwa kukosa virusi vya corona.

Hali hii iliipa afueni timu nzima ya wahudumu na wakasherehekea ushindi wa kwanza kabisa dhidi ya virusi vya corona Kaunti ya Nakuru.

Licha ya kwamba ugonjwa huo hauna tiba rasmi, waliweza kudhibiti dalili zote za wagonjwa hao wawili.

Siku tatu baadaye waliruhusiwa kwenda nyumbani ambapo waliendelea kujitenga kwa muda wa wiki moja kabla ya kutangamana na jamaa zao.

Kulingana na Bi Mosop, hali ya wagonjwa hao iliimarika kupitia dawa za kupunguza maumivu ya koo, joto mwilini na kikohozi, dawa za vitamini C, chakula bora, kuota jua na kunywa maji ya moto.

Wakati huu, hospitali hiyo ina mgonjwa mmoja ambaye anaendelea kupokea matibabu.

Watu wengi, zaidi ya 20 wapo kwenye karantini huku uchunguzi wa afya dhidi yao ukiendelea.