HabariSiasa

COVID-19: Ni juu yenu sasa!

July 7th, 2020 3 min read

NA WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatatu alilegeza masharti ya kukabiliana na virusi vya corona, akisema ameacha jukumu la kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo mikononi mwa kila Mkenya kibinafsi.

Rais alisema iwapo ulegezaji huo utachangia kuongezeka kwa maambukizi, basi hatasita kutangaza masharti hayo upya, kwa hivyo akataka kila mwananchi kutahadhari bila kungoja serikali kumlazimisha kufuata kanuni za kuzuia maambukizi.

“Serikali haitasita kuendelea kuchukua jukumu lake. Lakini tutashinda janga hili ikiwa kila mmoja wetu, mdogo ama mkubwa, mtoto hata mzee, mama ama baba atachukua jukumu lake kibinafsi,” akasema Rais alipohutubia taifa.

“Tusidanganyane kwamba ugonjwa huu hauko. Idadi yaendelea kupanda. Kwa hivyo jukumu lazima liwe ni la kila mtu.

“Kwa wale ambao watachukua nafasi hii kurudi mashambani, twasema pia hiyo ni sawa. Lakini ujue unarudi kwa nyanya na babu yako. Warudi kwa wazee na familia yako. Jukumu la kuwalinda sio la serikali.

“Kama wewe utawepelekea ugonjwa na hali unajua idadi ya wale wengi ambao wanaaga ni wazee, basi uamuzi ni wako. Sasa tumekupatia nafasi ya kusafiri. Waweza kwenda pahali popote, lakini ujue jukumu ni lako na ile shida ambayo itatokea kwao ujue wewe ndio umeipeleka.

“Nawaomba Wakenya, vile tulikuja pamoja wakati wa janga la Ukimwi, ambapo maelfu ya watu walikufa, mwishowe tuliweza kushinda kwa sababu kila mmoja alichukua jukumu lake.

“Hiyo ndio iliokoa maisha wala sio serikali. Serikali yaweza tu ikakueleza hatari ambayo iko mbele yako, lakini haiwezi kuwa katika nyumba yako ama kila kanisa, msikiti au soko kukulazimisha kutii masharti. Jukumu ni lako wewe mwenyewe.

“Ombi langu kwa Wakenya wenzangu ni kuwa twataka kuendelea kufungua nchi ili maisha yetu yarudi kawaida. Tuchukue nafasi hii kufanya yale ambayo yatatuwezesha sisi kama Wakenya kusonga mbele na kujiokoa kutokana na janga hili,” akasema Rais Kenyatta.

UHURU WA KUINGIA MIJINI

Katika kulegeza masharti ya kukabiliana na Covid-19, Rais Kenyatta aliondoa marufuku ya kuingia na kutoka kaunti za Nairobi, Mombasa na Mandera.

“Uamuzi wa kufungua usafiri maeneo haya una masharti. Iwapo hali itazorota tutarudisha marufuku. Tutafuatilia hali kwa siku 21 na tukiona dalili yoyote ya mambo kuharibika zaidi, hatutakuwa na lingine ila kufunga tena,” akasema Rais Kenyatta.

“Lakini ili tuweze kuendelea kufungua, lazima wewe binafsi ulinde ndugu yako. Jukumu hili ni la kila mtu binafsi. Hili sio jukumu la kutekelezwa na serikali. Ni wajibu wako kwa wananchi wenzako. Ni jambo la kujitolea kwa nia njema kwa jirani yako wakati wa furaha na wa matatizo. Ni jukumu la kujilinda wewe binafsi, familia yako na wengine,” akaeleza Rais.

Rais alihimiza Wakenya kuepuka safari zisizo muhimu mashambani, na kuendelea kuzingatia kanuni za kuzuia corona kama vile kuvaa barakoa, kunawa mikono na kuepuka misongamano.

SAFARI NYINGI MASHAMBANI

Kufuatia hatua hiyo, watu wengi ambao hawajaweza kusafiri mashambani kwa miezi mitatu iliyopita hasa nje ya Nairobi na Mombasa huenda wakaelekea mashambani kuona familia zao.

Hatua hiyo pia itawezesha kuunganishwa kwa familia ambazo zilitenganishwa marufuku hiyo ilipotangazwa mara ya kwanza mnamo Aprili 6 mwaka huu.

Kiongozi wa taifa alitangaza kuwa magari ya uchukuzi wa umma ya masafa marefu yatahitajika kuwa na vyeti vya kuonyesha yametimiza kanuni zote zinazohitajika.

Rais pia alitangaza kufunguliwa kwa maeneo ya ibada yakiwemo makanisa na misikiti, lakini kwa masharti makali, ambapo watoto walio chini ya miaka 13 na wazee walio na zaidi ya miaka 58 hawataruhusiwa kuhudhuria ibada.

Hata hivyo, kafyu inayoanza saa tatu jioni hadi saa kumi alfajiri itaendelea kote nchini kwa siku 30 zaidi.

Hii ina maana kuwa wanaosafiri watatakiwa kusafiri kati ya saa kumi alfajiri na saa tatu usiku.

Tangu marufuku ya kuingia hasa Mombasa na Nairobi, wenye magari ya uchukuzi wa umma, madereva na makanga wamekuwa na kipindi kigumu kifedha kwani hawajakuwa wakihudumu.

Baadhi walilazimika kugeuza magari yao kuwa ya kubeba mizigo katika juhudi za kujaribu kukabiliana na hali ngumu ya maisha.