Habari Mseto

COVID-19: Rais Kenyatta atarajiwa kutangaza hatima ya kafyu na zuio Jumamosi

May 15th, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta atawafahamisha Wakenya Jumamosi, Mei 16, 2020, ikiwa kafyu ya usiku kote nchini itaongezewa muda au la.

Vilevile, kiongozi wa taifa anatarajiwa kutangaza ikiwa amri ya kutotoka na kutoingia katika kaunti za Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale itasitishwa au itadumishwa.

Hatua za mwanzo kiongozi wa nchi alizitangaza Machi 27, 2020, ambapo aliagiza zuio hilo la usafiri kwa siku 21 na mnamo Aprili 25, 2020, akatangaza kurefushwa kwa agizo hilo kwa siku 21 zaidi ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

“Jinsi mnavyofahamu, muda wa kutekelezwa wa baadhi ya masharti yaliyowekwa unaelekea kumalizika. Na suala hili sasa linazungumziwa. Kesho (Jumamosi) taarifa kamili kuhusu masharti hayo itatolewa,” Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman amewaambia wanahabari Ijumaa katika makao makuu ya wizara hiyo, Nairobi.

“Taarifa hiyo itatolea na Mheshimiwa Rais katika Hotuba kwa Taifa kesho (Jumamosi),” ameeleza.

Serikali ilitangaza amri ya kutotoka nje na kuingia katika kaunti hizo nne baada ya kubaini kama ndivyo vitovu vya kusambaa kwa virusi vya corona.

Hata hivyo, kufikia sasa kaunti za Nairobi na Mombasa bado zinaendelea kuandikisha idadi kubwa ya maambukizi mapya.

Eastleigh na Mji wa Kale

Ni kutokana na hali hiyo ambapo maeneo ya Eastleigh (Nairobi) na Mji wa Kale – Old Town – (Mombasa) yalifungwa Jumatano wiki jana kwa lengo la kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

Wizara imewapongeza wakazi wanaoishi mitaa ya Eastleigh na Mji wa Kale kwa kukubali kujitokeza kukaguliwa na kupimwa ugonjwa wa Covid-19.

Mnamo Mei 6, 2020, mitaa hiyo iliwekewa kafyu ya wiki mbili mfululizo kwa sababu ya idadi ya juu ya maambukizi ya virusi vya corona.

Shughuli za kuingia na kutoka humo zilisimamishwa.

Wizara imeeleza kuridhishwa kwake na ushirikiano wa wakazi wa mitaa hiyo kujitokeza kupimwa Covid-19.

“Wakazi wa Eastleigh jijini Nairobi na Mji wa Kale, Mombasa, ninawapongeza kwa ushirikiano mlioonyesha kujitokeza kupimwa,” amesema Dkt Aman.

Hali yaelekea kuwa nzuri katika kaunti za Kilifi na Kwale kwa sababu hazijagonga vichwa vya habari katika siku za hivi karibuni kuhusiana na kutokea kwa visa vipya vya maambukizi.

Mnamo Jumanne Gavana wa Kilifi Amason Kingi alisema kuwa watu wote sita kutokana kaunti hiyo ambao walikuw wakitibiwa wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumba “na hatujashuhudiwa visa vingine.”

“Hata hivyo, bado tunawahimiwa raia kuendelea kutii masharti yaliwekwa na serikali ili tuweze kuzima kabisa janga hili,” akawaambia wanahabari.