Habari

COVID-19: Seneta alisha mifugo na kutazama wanyamapori

April 30th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

SENETA wa Lamu, Anwar Loitiptip ameonekana kutii kwa njia tofauti maelekezo ya serikali kupitia Wizara ya Afya kuhusiana na jinsi wananchi wanavyostahili kujiweka ili kuzuia kuenea kwa maradhi ya coronavirus nchini.

Juma hili, Bw Loitiptip alionekana akichunga mifugo yake ikiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo katika eneo mojawapo la mashambani.

Bw Loitiptip alisema aliamua kutoka jiji la Nairobi na kuja kukaa mashambani kulisha mifugo na hata kuangalia wanyamapori kama mbinu mojawapo ya kutii amri ya kukaa nyumbani na kuzuia mtagusano wakati huu ambapo serikali na ulimwengu unakabiliana dhidi ya janga la Covid-19.

Seneta huyo kijana na ambaye katika siku za hivi punde ameibukia kupenda mifugo na wanyamapori pia alionekana akitazama wanyama mwitu mbuga moja kwenye maeneo ya Mkunumbi na Milihoi, Kaunti ya Lamu.

Bw Loitiptip pia alionekana sehemu mojawapo ya ufukwe wa Bahari Hindi eneo la Lamu akicheza na mbwa wake.

“Niliamua kuja kijijini kwetu na kulisha mifugo kama njia mojawapo ya kutii maelekezo mbalimbali ya Wizara ya Afya, ikiwemo kuepuka misongamano, mitagusano na pia kuweka umbali ufaao kati ya mtu na mwingine,” akasema Bw Loitiptip.

Aliongeza kuwa akilisha mifugo pia anapata fursa mwafaka ya kutafakari jinsi taifa linavyoelekea kama taifa na nafasi kutazama wanyamapori eneo la Lamu.

“Tuko na rasilimali chungu nzima hapa Lamu,” akasema.

Seneta huyo aidha amewataka viongozi wenzake wa kisiasa kuepuka kuandaa mikutano ya hadhara msimu huu wa janga la Covid-19 na badala yake kutii maelekezo yote yanayotolewa na Wizara ya Afya ili kudhibniti kuenea kwa maradhi hayo hatari.

Bw Loitiptip kadhalika amewashauri vijana kuwa mstari wa mbele katika kuielimisha jamii nchini kuhusiana na janga la corona.

Pia amewataka kutii sheria zote zinazoambatana na vita dhidi ya coronavirus na akawaonya dhidi ya kujihusisha na ulevi usiokuwa na maana.

Kauli ya Bw Loitiptip inajiri siku chache baada ya Mshirikishi wa Usalama Ukanda wa Pwani, Bw John Elungata kuwaonya wanasiasa wa Kaunti sita za Pwani, hasa wale wa Lamu na Tana River dhidi ya kwenda kinyume na maelekezo ya serikali kuhusu janga la corona.

Bw Elungata alisema ofisi yake tayari ilikuwa ikiwachunguza wabunge, maseneta na wawakilishi wa wanawake kwenye kaunti husika wanaodaiwa kuzunguka vijijini kwa madai kwamba wanatoa misaada kwa umma ambacho ni kinyume cha maelekezo yaliyopo ya serikali.

“Misaada yote inayotolewa kwa minajili ya kuwapa waathiriwa wa janga la Covid-19 lazima ipitie kwa kamati za kaunti kuhusu janga hilo. Kamati hizo zinaongozwa na kamishna wa kaunti na gavana. Ikiwa kuna yeyote anayeenda kinyume na maelekezo hayo basi tutamkamata na kumtupa kwenye karantini ya lazima,” akasema Bw Elungata.