Habari Mseto

COVID-19: Serikali kulipia upimaji wa wahudumu wa hoteli

April 28th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imewaondolea waamiliki ya mikahawa na hoteli mzigo kwa kutangaza italipia gharama ya wafanyakazi wao kupimwa virusi vya corona kabla ya wao kuruhusiwa kurejea kazini.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Afya Dkt Patrick Amoth ameongeza kuwa serikali pia ndiyo inagharimia mpango unaoendelea sasa wa kuwapima madereva wa matrela katika mipaka ya Kenya na mataifa jirani, kubaini ikiwa wanavirusi vya corona.

“Ningependa kuwahakikishia wamiliki ya wa mikahawa na hoteli kwamba serikali italipia gharama ya kupimwa kwa wafanyakazi wao. Hii ni kwa sababu serikali ndio imetangaza kufunguliwa kwa biashara hizo, japo kwa kufuata mwongozo mpya uliotangazwa na Wizara ya Afya wa ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona,” Dkt Amoth akasema kwenye mahojiano na runinga ya Citizen Jumatatu usiku.

Afisa huyo alishauri watu wanaotaka kupimwa virusi vya corona kutembelea vituo vya Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu Nchini (KEMRI), Nairobi na Kisumu, National Influenza Centre, Nairobi, Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH), Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) Eldoret na Hospitali ya Rufaa ya Pwani na ile ya Nyeri.

“Vile vile, huduma za kupima washukiwa wa Covid-19 vinapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Wajir ambayo itahudumia eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya,” Dkt Amoth akaongeza.

Saa chache baada ya serikali kutangaza kuwa itaruhusu kufunguliwa kwa mikahawa na hoteli mradi wamiliki wazingatie masharti kadha ikiwemo kupimwa kwa wafanyakazi wao, baadhi ya wamiliki wa biashara hiyo mjini Nakuru walilalamikia gharama ya juu ya huduma hiyo.

Mnamo Jumatatu Nairobi Hospitali ilitangaza kuwa itaanza kutoa huduma za kupima virusi vya corona lakini kwa gharama ya Sh10,000.

Wakati huo huo, Dkt Amoth ameelezea matumaini kuwa kero la msongamano ya matrela kutokana na kucheleweshwa kwa shughuli za kuwapima wahudumu, litapungua wiki hii baada ya serikali kupokea vifaa 40,000 vya kuendesha shughuli hiyo.