Habari Mseto

COVID-19: Serikali kuwalinda wauguzi

June 26th, 2020 1 min read

Na JUMA NAMLOLA

SERIKALI itaendelea kuwalinda wauguzi, kama njia ya kuendeleza juhudi za kukabili maambukizi ya maradhi ya Covid-19.

Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Mercy Mwangangi, alisema sehemu ya juhudi hizo ni kuhakikisha kwamba wauguzi wanapata vifaa muhimu vya kuwakinga.

Dkt Mwangangi alitangaza maambukizi mapya 178, yaliyofikisha idadi ya maambukizi yote nchini kuwa 5,384 tangu Machi.

“Nairobi inaongoza kwa visa 100 vya wagonjwa walioambukizwa virusi hivi, ikifuatwa na Migori yenye visa 21,” akasema.

Kaunti nyingine zilikuwa Kiambu (16), Busia (8), Mombasa (7), Machakos (4), na Nakuru (2). Kaunti za Uasin Gishu, Taita-Taveta na Kericho zikiwa na kisa kimoja kila moja.

Wagonjwa wengine wawili walifariki Alhamisi na kufikisha idadi ya vifo kutokana na corona kuwa 132.

Hata hivyo, watu 34 waliokuwa wakiugua walipona na kuruhusiwa kuondoka kutoka vituo vya matibabu.