Habari Mseto

COVID-19: Serikali yafunga Mandera

April 23rd, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imetangaza marufuku ya watu kuingia na kutoka kaunti ya Mandera kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona katika kaunti hiyo.

Akitoa taarifa ya kila siku kuhusu hali ya janga hilo Waziri wa Afya Mutahi Kagwe Jumatano alisema kuwa kati ya watu saba wapya waliothibitishwa kuwa virusi hivyo, wawili wanatoka Mandera, na ni wakimbizi.

Hiyo inafikisha wanane (8) watu wanaogua ugonjwa wa Covid-19 katika kaunti hiyo inayopakana na taifa la Somalia.

“Kwa hivyo, leo Serikali imepiga marufuku watu kuingia na kutoka kaunti ya Mandera kwa sababu imebainika kuwa hatari zaidi,” Bw Kagwe akawaambia wanahabari katika makao makuu ya Wizara ya Afya, Nairobi.

Kulingana na Kagwe, visa hivyo vipya saba sasa vinafikisha idadi jumla ya visa vya maambukizi nchini kuwa 303.

Alitoa tangazo hilo dakika chache baada ya mwenzake wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’I kutoa tangazo kama hili kwenye ujumbe kupitia mtandao wa twitter.

“Kufuatia kusambaa kwa kasi kwa ugonjwa wa Covid-19 katika kaunti ya Mandera, serikali imeamuru kusitishwa kwa safari za kuingia na kutoka humo, kupitia barabarani au angani, kwa kipindi cha siku 21 kuanzia saa moja jioni leo (Jumanne)-Aprili 22, 2020,” akasema Bw Matiang’i.

Mandera sasa inaungana na kaunti za Nairobi, Kilifi, Mombasa na Kwale kama zile ambako amri hiyo inatekelezwa.

Hivi majuzi, watu 32 walitoroka. Kwa njia ya kutatanisha, kutoka karantini ya lazima walikofungiwa katika eneo la Elwak.

Watu hao walikuwa miongoni mwa wengine 66 ambao walikuwa wamesafiri kutoka Nairobi.