Makala

COVID-19: Ubalozi wa Iran na washirika wazindua jukwaa la wachoraji vibonzo kuonyesha weledi wao

May 27th, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

UGONJWA wa Covid-19 ambao uliripotiwa kwa mara ya kwanza Wuhan katika mkoa wa Hubei nchini China mwishoni mwa mwaka 2019, umegeuka kuwa janga la kimataifa.

Ni janga ambalo limekuwa kero katika kila kona ya ulimwengu, kutokana na athari zake katika uchumi. Si sekta ya biashara, si elimu, si utalii, si kilimo, si uchukuzi; chache tu kuziorodhesha, zote zinahisi makali ya Covid-19.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani, ndilo WHO, ugonjwa huu hautaisha hivi karibuni, hivyo basi watu wajiandae kuishi nao kwa muda usiojulikana, huku madaktari na Wanasayansi wakiwa mbioni kutafuta chanjo na tiba.

Maambukizi ya Covid-19 hayabagui taifa wala tabaka, tajiri wala maskini.

Kila taifa limeweka mikakati na sheria kudhibiti msambao wa virusi hatari vya corona, vinavyosababisha ugonjwa huu.

Nchini Kenya, uvaliaji maski hasa maeneo ya umma, kudumisha kiwango cha usafi kwa kunawa mikono na kuzingatia umbali kati ya mtu na mwenzake, ni baadhi ya mikakati iliyowekwa na Wizara ya Afya.

Kulingana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya nchini, Dkt Patrick Amoth, amri ya kuingia na kutoingia baadhi ya kaunti pamoja na kafyu ya kati ya saa moja za jioni hadi saa kumi na moja za asubuhi, imechangia kudhibiti maenezi zaidi Kenya.

“Tulikuwa tumetabiri maambukizi ya visa 10, 000 kufikia mwishoni mwa Aprili 2020 ila kafyu tuliyoweka ilisaidia kudhibiti,” Dkt Amoth akasema katika kimojawapo cha vikao na wanahabari.

Sawa na mabara mengine duniani, Afrika ina wajibu mkuu kuzuia msambao wa Covid-19.

Uchumi wa Afrika haujaimarika kiasi cha kujigamba, ikizingatiwa kuwa mataifa mengi yangali yanapitia wakati mgumu kustawisha sekta ya afya na la mno kukithi raia wake mahitaji muhimu ya kimsingi.

Licha ya nchi za Afrika kukaza kamba kuzuia maenezi, mamilioni ya watu wanaendelea kuathirika kwa njia moja au nyingine.

Kitendawili kilichoko ni mikakati itakayowekwa kunusuru waathiriwa. Aidha, hilo linaenda sambamba na ni; Chombo kipi kitatumika kwa muda wa miezi sita, mwaka mmoja au miaka kumi ijayo kufanya hamasa ya athari za Covid – 19, namna ya kudhibiti msambao wakati huu na baadaye?

Ni jukumu la viongozi, taasisi husika pamoja na mashirika na walioko mamlakani kutumia fursa zilizopo kufanya hamasisho. Sanaa ni mojawapo ya njia ya mawasiliano inayotumika kupasha ujumbe.

Kimaelezo, sanaa ni ufundi anaoutumia mwanadamu ili kuwasilisha fikra au mawazo yaliyo ndani ya akili yake.

Ni zana ya mawasiliano iliyogawanywa kwa msingi wa makundi kadhaa, kuanzia uchoraji wa picha, vibonzo, michezo ya kuigiza pia drama, nyimbo, mashairi kwa njia ya kughani au kuimba, sarakasi, miongoni mwa sanaa zingine.

Kando na kuhamasisha, sanaa inapendekeza suluhu kwa njia ya ucheshi, hususan katuni zinazoelimisha, fahamisha na kuvunja mbavu mashabiki, ambao ni umma unaolengwa.

Ili kufanya hamasisho kudhibiti msambao wa Covid-19 Barani Afrika kipindi hiki kigumu na baada, Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapa nchini Kenya umezindua Tamasha za Katuni Afrika, zitakazotumia kazi za sanaa.

Kwa ushirikiano na wadau husika wanaojumuisha Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) na Muungano wa Katuni Afrika Mashariki, Ubalozi huo unasema jukwaa hilo litawezesha vipaji katika sekta ya sanaa Afrika kuonesha umahiri wao kwa njia ya hamasisho kuangazia janga la corona na mikakati maalum kuzuia ueneaji zaidi.

Katika mukhtadha huu, wasanii hasa vijana, wanatakiwa kutumia talanta zao kuonyesha taswira halisi ya mambo yalivyo, tunachopaswa kufanya kama vile kufuata taratibu na sheria zilizowekwa na idara ya afya, na tathmini ya siku za usoni, chini ya janga hili kuu.

Akipokea habari hii njema, Paul Kahiro, mratibu wa mikakati katika kundi la kijamii la Liberty, linalotumia sanaa kuhamasisha umma kuhusu athari za ugonjwa wa Ukimwi, matumizi ya dawa za kulevya na vilevile mihadarati katika kaunti ya Nairobi na viunga vyake, anasema ubunifu unapaswa kuwa wa kipekee na wa aina yake.

Kundi la Liberty, linalotumia sanaa kuangazia athari za Ukimwi, dawa za kulevya na mihadarati. Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapa nchini Kenya umezindua Tamasha za Katuni Kiafrika, matumizi ya sanaa kuangazia Covid-19. Picha/ Sammy Waweru

“Covid-19 ni janga la kimataifa, ambapo sanaa kuliangazia inapaswa kuvutia umma kwa njia ya ucheshi. Iwe kwa matumizi ya vibonzo kuigiza, michezo ya kuigiza, mashairi, michoro, nyimbo, au sanaa yoyote ile, stori (akimaanisha utunzi wa mtungo) inapaswa kuwa ya hadhi yake na ya kuvutia watu ili kupasha ujumbe,” Paul ambaye pia ni DJ anafafanua.

Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu Iran Kenya ulitangaza kuzindua Tamasha za Katuni Afrika kuangazia janga la Covid-19 Afrika, siku moja baada ya Bara la Afrika kuadhimisha Sikukuu ya Waafrika, inayoadhimishwa Mei 25 kila mwaka.

Aidha, tamasha hizo zinaendelea hadi Agosti 24, 2020, wasanii wakitakiwa kuwasilisha kazi zao kupitia anwani ya baruapepe: [email protected] ambapo lugha zinazopendekezwa ni Kiingereza, Kiswahili, Kiarabu, Kireno, Kifaransa na Persian.

Kama ilivyosimama kidete na mataifa ya Bara Afrika kutetea Uhuru wa Kujitawala, pamoja na kuimarisha uchumi na miradi ya maendeleo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imeahidi kusima imara na Afrika wakati huu mgumu wa Covid-19 na hata baada ya janga hili.