Habari

COVID-19: Viongozi Mombasa wawatunuka sifa vijana kwa kazi nzuri ya kuhamasisha umma

August 13th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

VIJANA Mombasa wamepongezwa kwa kazi nzuri ya kutoa hamasisho kuhusu Covid-19 na hivyo kusaidia kupungua kwa visa vya corona katika kaunti hiyo.

Akizungumza na vijana hao Jumanne katika hafla ya kusherehekea siku ya kimataifa ya vijana katika majengo ya SwahiliPot, Mombasa, Afisa Mkuu wa Afya ya Umma katika kaunti ya hiyo, Bi Aisha Abubakar alisema juhudi za vijana kuhamasisha wanajamii kuhusu janga la corona zimezaa matunda “kwa sababu ni watu wachache wanaoambukizwa maradhi ya Covid-19”.

“Vijana wakishirikia na maafisa wa afya ya jamii wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wakazi jinsi ya kujikinga na janga hili. Namba zetu zimeenda chini kwa sababu ya vijana hao kuhamasisha umma,” akasema Bi Aisha.

Kaunti ya Mombasa ni mojawapo ya kaunti ambazo idadi ya watu wanaoambukizwa ugonjwa wa Covid-19 kwa kuzingatia takwimu za kila siku, imepungua pakubwa ikilinganishwa na miezi michache ambayo imepita.

Hapo awali, kaunti ya Mombasa ilikuwa miongoni mwa kaunti zilizorekodi idadi kubwa ya watu wenye maradhi ya Covid-19, hali iliyomlazimu Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku kuingia na kutoka kwa kaunti hiyo, ili kuzuia maambukizi zaidi.

Kaunti zingine ‘zilizofungwa na kufunguliwa’ ni Nairobi na Mandera.

Waziri wa Afya katika kaunti hiyo, Dkt Khadija Shikely naye aliwapongeza vijana kwa kuzingatia hatua zilizowekwa na Wizara ya Afya kama vile kuvalia barakoa na kutokaribiana – kwa kuweka umbali wa mita moja au zaidi – ili kuzuia maambukizi ya corona.

Dkt Shikely alithibitisha kuwa kazi nyingi katika sekta ya hiyo zinafanywa na watu wazee na sasa vijana wengi wanahitajika, iwapo wahudumu hao watastaafu.

Aliongeza kuwa kuwa kazi katika sekta ya afya zipo, ni vijana tu wanaotakikana kujisajilisha katika kozi kama vile uuguzi, lishe, maabara na kadhalika.

“Kazi zipo na tunahitaji vijana wengi waje wakazifanya,” alisema Dkt Shikely huku akisema kuwa uvumbuzi wowote unaolenga idara ya afya utapigwa jeki.

Pia, aliwaomba wahudumu wa afya waliostaafu waweze kuwa mstari wa mbele kuwapa vijana mafunzo ili nao wapate fursa ya kuendeleza ujuzi wao “ndipo mwananchi wa kawaida asaidike.”

“Tunawaomba mnapostaafu, msiende nyumbani kabisa bali mtumie fursa hiyo kuwapa vijana mafunzo zaidi,” akasema.