Habari

COVID-19: Visa 22 vipya, 22 wapona huku kukiwa na vifo vya watu wanne

May 13th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WATU 22 zaidi wamepatikana na virusi vya corona nchini na kufikisha idadi jumla ya visa hivyo nchini kufikia leo Jumatano kuwa 737 huku wagonjwa wanne wakifariki.

Wizara imesema wawili wamefariki jijini Nairobi huku mmoja akifariki mjini Mombasa na mwingine katika Kaunti ya Bomet.

Idadi ya wale ambao wamefariki kutokana na maradhi ya Covid-19 nchini Kenya sasa imefika wahanga 40.

Visa hivyo vipwa viligunduliwa baada ya sampuli 1,516 kufanyiwa uchunguzi ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita.

Akitoa taarifa ya kila siku kuhusu hali ya ugonjwa huo nchini, Waziri Msaidizi wa Afya (CAS) Dkt Rashid Aman hata hivyo ametoa habari njema ya wagonjwa 22 zaidi kupona.

Hii ina maana kuwa waliopona na kuruhusiwa kwenda nyumbani kufikia sasa idadi yao imefika 281.

“Miongoni mwa wagonjwa hao 22 wapya 10 wanatoka Nairobi, wanane wanatoka Mombasa, watatu kutoka Kajiado na mmoja kutoka Bomet,” akasema Dkt Aman nje ya makao makuu ya Wizara ya Afya jijini Nairobi.

Waziri huyo msaidizi amewaonya wafanyabiashara hasa katika maeneo ya Pwani dhidi ya kuongeza bei za bidhaa za kimsingi kiholela.

“Ni makosa kwa wenye maduka kuongeza bei za vyakula na bidhaa zingine za kimsingi wakati huu mgumu ambapo kila aghalabu kila raia na hata kila mtu duniani anahisi athari hasi za homa ya corona kwa njia moja ama nyingine,” akasema.