Habari Mseto

COVID-19: Visa jumla nchini Kenya sasa ni 1,029

May 20th, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

VISA vya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 sasa vimevuka 1,000 baada ya visa 66 kuthibitishwa katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Idadi hiyo ya visa vipya ni ya juu zaidi kuwahi kuthibitishwa katika kipindi hicho tangu mlipuko wa virusi vya corona nchini ulipothibitishwa kwa mara ya kwanza nchini Kenya mnamo Machi 13, 2020.

Idadi jumla ya visa sasa ni 1,029.

Akitoa takwimu hizo Jumatano katika makao makuu ya Wizara ya Afya, Nairobi, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema wagonjwa 64 wapya ni Wakenya ilhali wawili ni wageni.

Nairobi na Mombasa zinaendelea kuongoza katika visa vya maambukizi.

Kati ya visa hivyo, 30 ni vya Mombasa ilhali wengine 26 wanatoka Nairobi.

Pia ameitaja Kaunti ya Kajiado akielezea wasiwasi wake.

“Na watu wawili wanatoka katika Kaunti ya Kajiado. Hii ni kwa sababu wakati huu eneo la Namanga linashuhudia ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona kutokana na uwepo wa madereva wa matrela ya masafa marefu kutoka Tanzania,” Bw Kagwe amesema.

Kafyu yarefushwa Eastleigh na Mji wa Kale

Waziri pia amesema amri ya kuzuia watu kuingia au kutoka katika mtaa wa Eastleigh, Nairobi na Mji wa Kale, Mombasa itaendelea kwa muda wa wiki mbili zaidi.

Kagwe ameongeza kwa muda wa kafyu hiyo hadi mnamo Juni 6, 2020.

“Amri ya kutoingia na kutotoka mtaa wa Eastleigh na Mji wa Kale itaendelea hadi Jumamosi, Juni 6, 2020,” Bw Kagwe akasema.

Waziri pia amesema maabadi yatasalia yamefungwa hadi muda wa kafyu uliowekwa ukamilike.

“Hoteli, maduka ya kuuza nguo, masoko na uchuuzi; shughuli hizi zote bado zimesitishwa,” akasisitiza, akisema hatua hiyo itasaidia kuzuia msambao wa Covid-19 katika mitaa hiyo.

Mitaa hiyo miwili ilifungwa mnamo Mei 6, 2020, kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona, amri iliyotarajiwa kufikia kikomo leo Jumatano.

Amri ya kutoingia na kutotoka Eastleigh na Mji wa Kale, inaendelea huku ile ya kitaifa ya kafyu ya saa moja jioni hadi saa kumi na moja asubuhi kila siku pia ikiendelea kutekelezwa.

Wakazi wa mitaa hiyo hata hivyo wamekuwa na malalamiko ya hali ngumu ya maisha, hasa kukosa chakula na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.