Habari

COVID-19: Visa nchini vyakaribia 8,000

July 5th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

JUMLA ya watu 309 zaidi Jumapili wamethibitishwa kuwa na virusi vya corona baada ya sampuli 4,228 kutoka kaunti 37 kupimwa ndani ya muda wa saa 24 zilizopita.

Mgonjwa mdogo zaidi ni mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja huku mkubwa zaidi mwenye akiwa na umri wa miaka 89.

Miongoni mwao 302 ni Wakenya ilhali saba ni raia wa kigeni na 217 ni wa jinsia ya kiume huku 92 wakiwa wa jinsia ya kike.

Kwa mara nyingine Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa kuandikisha visa vipya 193 Kajiado ikifuatia na visa 22. Mombasa ni nambari tatu kwa visa 18, Kiambu (20) huku kaunti za Makueni, Busia na Machakos zikiandikisha visa vipya 17, 11, na tisa mtawalia.

Kaunti za Nandi na Turkana zimeandikisha visa vitatu kila moja huku Narok, Nyandarua, Kakamega na Kilifi zikiripoti kisa kimoja kila moja.

Wakati huo huo, kiwango cha vifo kutokana na Covid-19 nchini kimepungua hadi asilimia 2.3 tangu kuripotiwa kwa mlipuko wa ugonjwa huo nchini mapema mwezi wa Machi mwaka.

Kifo cha hivi punde ni cha mtu mmoja aliyeathirika na kimeripotiwa Jumapili jioni na kufikisha 160 idadi jumla ya vifo. Na watu 309 zaidi waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya corona wanafikisha 7,886 idadi jumla ya maambukizi.

Mnamo mwezi wa Aprili kiwango cha vifo kutokana na Covid-19 kilikuwa asilimia 5.1 kwa wastani. Baadaye kiwango hicho kilishuka hadi asilimia 3.4 mnamo Mei na kuteremka zaidi hadi asilimia 2.5 mwezi wa Juni.

Akitoa taarifa kuhusu hali ya janga hili nchini, Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman pia amesema kuwa wagonjwa 51 zaidi wamepona na kuondoka hospitalini. Hii ina maana kuwa kufikia Jumapili jumla ya watu 2,287 walikuwa wamepona tangu kisa cha kwanza kuripotiwa nchini.

Kiwango cha wagonjwa ambao wanapona kimefika asilimia 29 ya idadi jumla ya walioambukizwa.

“Tungependa kuwapongeza wahudumu wetu wa afya ambao bidii na kutolea kwao kazini vimetuwezesha kupata ufanisi huu,” Dkt Aman amesema.