Habari

COVID-19: Visa vipya 188

September 13th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WIZARA ya Afya kwa mara nyingine Jumapili, Septemba 13, 2020, imekwepa kuwaita wanahabari kwa kikao cha kutoa maelezo kuhusu hali ya janga la Covid-19.

Ni kipindi ambacho mienendo na wanasiasa kukaidi masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona imekuwa ikishuhudiwa.

Waziri Mutahi Kagwe na wasaidizi wake Mercy Mwangangi na Rashid Aman pia wanaonekana kuogopa maswali magumu kutoka kwa wanahabari kuhusu sakata za ubadhirifu wa fedha za umma katika ununuzi wa vifaa vya kupambana na janga hilo, inayoizonga Mamlaka ya Ununuzi Dawa na Vifaa vya Kimatibabu Nchini (Kemsa)

Badala yake waziri ametuma taarifa kwa vyombo vya habari yenye takwimu kuhusu hali ya ugonjwa huo nchini ambapo visa 188 vimenakiliwa ndani ya saa 24 na hivyo kufikisha idadi jumla ya maambukizi kuwa 36,157

Visa hivyo vipya vimegunduliwa baada ya sampuli 3,092 kupimwa, na hivyo kufikisha idadi ya sampuli zilizopimwa nchini tangu Machi 13, 2020, kuwa 497,652.

Wakati huo huo, waziri Kagwe amesema wagonjwa watatu zaidi wamefariki kutokana na Covid-19 na hivyo kufikisha 622 idadi ya maafa kufikia Septemba 13, 2020.

Kaunti ya Mombasa imenakili idadi kubwa ya visa hivyo vipya, kwa kuchangia wagonjwa wapya 43 ikifuatwa na Turkana yenye visa 29.

Trans-Nzoia imeandikisha visa vipya 27, Nairobi (23), Kiambu (10), Nakuru (7), Kjiado (7), Uasin Gishu (5), Kilifi (5), Embu (5), Kisumu (4), Kericho (4) na Taita Taveta visa vinne (4).

Navyo visa viwili vimethibitishwa katika kaunti ya Kitui, Nyeri (2), Laikipia (2), Meru (2) huku Narok, Machakos Lamu, Samburu, Tharaka Nithi , Garissa na Kakamega zikinakili kisa kimoja kila moja.

Wizara hiyo pia imetangaza kuwa jumla ya wagonjwa 296 wamethibitishwa kupona, 28 wakiwa ni wale waliokuwa wakitunzwa nyumbani ilhali 268 ni wale waliokuwa wakipokea matibabu katika hospitali mbalimbali nchini.

Kwa hivyo, idadi jumla ya waliopona imefika 23,067.

Wakenya wamekuwa wakishangaa ni kwa nini Wizara ya Afya inaendelea kuwahimiza kufuata masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona kama vile kutotangamana, ilhali wanasiasa wamekuwa wakikusanya watu katika mikutano mikubwa ya kisiasa.

Wamiliki wa baa na wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma sasa wanaitaka serikali kuwaruhusu kuendelea na biashara zao kama kawaida kwani “inaonekana hata wanasiasa wameng’amua kuwa corona haipo tena.”