Habari

COVID-19: Visa vipya 278 idadi jumla ikifika 5,811

June 27th, 2020 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

SERIKALI imeonya kwamba visa vya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 vinatarajiwa kwenda juu zaidi nchini.

Waziri Msaidizi wa Afya (CAS) Dkt Mercy Mwangangi amesema hayo Jumamosi ambapo amethibitisha visa vipya 278 vya maambukizi ya Covid-19 vikiripotiwa katika saa 24 zilizopita.

Visa hivyo vimeripotiwa baada ya ukaguzi wa sampuli 4,074 kutoka sehemu mbali mbali nchini.

“Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa visa 172 huku ile ya Mombasa ikifuatia kwa visa 37,” amesema Dkt Mwangangi.

Sasa kuna jumla ya visa 5,811 vilivyothibitishwa nchini.

Dkt Mwangangi ameonya kwamba idadi ya watoto wachanga wanaoambukizwa kila siku inaendelea kuongezeka.

“Ni jukumu la wazazi hasa akina mama wenye watoto wadogo kuzingatia sheria zilizowekwa za kuzuia maambukizi haya,” ameongeza Dkt Mwangangi.

Watu wanne wameripotiwa kufariki kutokana na ugonjwa huo katika kipindi cha saa 24 wanafanya idadi jumla ya wahanga kufika 142 nchini.