Habari

COVID-19: Visa vipya 421 vyafikisha 11,673 idadi jumla

July 16th, 2020 2 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

VISA 421 vipya kutokana na sampuli 3,895 katika kipindi cha saa 24 zilizopita vinafikisha 11,673 idadi jumla ya wagonjwa wa Covid-19 nchini, Waziri  wa Afya Mutahi Kagwe amesema Alhamisi akiwa mjini Nakuru.

Kati ya 421 hao, 409 ni Wakenya huku 12 wakiwa raia wa nchi za kigeni.

Waziri Kagwe amebainisha wagonjwa 297 ni wa kiume na 124 wa jinsia ya kike.

Aidha, mgonjwa wa umri wa chini zaidi ni mtoto mwenye umri wa miaka mitatu huku wa umri wa juu akiwa mwanamume mwenye umri wa miaka 93.

Bw Kagwe ametangaza hayo akiwa Kaunti ya Nakuru ambapo pia amezindua huduma ya afya ya msingi.

Amesema Nairobi inaongoza kwa maambukizi kwa kurekodi zaidi ya watu 6,000 tangu kisa cha kwanza kufikia sasa ikifuatwa na Mombasa ilio na watu zaidi ya 1,000 na kisha Kaunti ya Kiambu (640).

Watu wanane zaidi wameaga dunia na kufanya 217 idadi ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Kaunti ya Nakuru imeripoti jumla ya visa 155 huku wengi wa wagonjwa wakiwa madereva wa matrela. Hata hivyo, zaidi watu 30 wametibiwa na kupona.

Kulingana na Bw Kagwe, huduma za utunzaji wa nyumbani hasa kwa wagonjwa wasioonyesha dalili, zitasaidia kupunguza msongamano katika hospitali za humu nchini.

“Serikali iko tayari kutoa msaada wake ili kufanikisha huduma hizi wa wakenya wote. Sasa ni jukumu la kaunti zote kujitokeza na kuunga mkono mradi huu,” akasema waziri Kagwe.

Bw Kagwe amesema tayari serikali imeteua wahudumu wa afya wa kujitolea 31,780 ambao pia wameshapata mafunzo jinsi ya kuwezesha huduma za matibabu ya nyumbani vijijini.

“Kaunti tayari zimebuni mfumo mpya wa huduma za msingi ambao utatumika kwa muda wa mwaka wa 2020/2021. Itakuwa vyema ikiwa kaunti hizo zitafanya hima kuunga mkono juhudi hizi,” akasema Bw Kagwe.

Waziri huyo ameonya maabara za wamiliki binafsi ambazo zinaendesha vipimo vya ugonjwa wa Covid-19 na kisha kutoa matokeo tatanishi, kwamba vituo hivyo vitapokonywa leseni.

Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui amepongeza juhudu za Wizara ya Afya na kuwataka wakazi kuzingatia kanuni zilizowekwa ili kujikinga na maambukizi.

Kulingana naye, kati ya maambukizi yaliyoripotiwa Nakuru, asilimia 73 ni watu wa jinsia ya kiume huku asilimia 27 wakiwa wagonjwa wa kike.

“Kaunti ya Nakuru tayari inazingatia huduma za nyumbani kwa wagonjwa ambao wamepatikana na virusi vya corona lakini hawaonyeshi dalili zozote. Jumla ya wagonjwa 26 wanatibiwa nyumbani katika maeneo tofauti,” akasema Bw Kinyanjui.

Kaunti ya Nakuru sasa inatazamia kuwa na vitanda 1,000 vilivyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa Covid-19 baada ya jengo la ghorofa tatu lilionuiwa awali kuwa la wagonjwa kufika kutibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani, kukaribia kukamilika kwa muda wa wiki nne zijazo.