Habari

COVID-19: Visa vipya leo ni 25 idadi jumla nchini ikifika 607

May 7th, 2020 1 min read

Na MWANDISHI WETU

VISA vipya vya Covid-19 nchini Kenya leo Alhamisi ni 25 idadi jumla nchini ikifika 607, ametangaza Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Rashid Aman.

Katika takwimu hizo zilizotangazwa katika makao makuu ya wizara jijini Nairobi, imebainika 22 ni Wakenya, mmoja kutoka Uganda, mwingine ni Mtanzania halafu mwingine ni Mchina.

Waliopona kufikia sasa ni 197 nao wahanga walioangamia idadi yao imepanda na kufika watu 29.

Dkt Aman amesema hayo baada ya kuthibitisha kwamba idadi ya hivi punde ya waliofariki ni ya wagonjwa watatu ambapo wawili ni wa jijini Nairobi, huku mwingine akiwa wa Mombasa.

“Ninawahimiza mfuate kanuni na ushauri wa kiafya kikamilifu; ukiwa katika eneo la janga la maradhi haya usiondoke, na ukisikia kuna janga pahala fulani, usiingie,” ameshauri Dkt Aman.

Serikali imewataka raia wa maeneo ya mipakani, hasa Migori na Isiolo waisaidie kudhibiti mianya ambayo watu kutoka Tanzania na Somalia mtawalia wanaingia na hivyo kuyaweka maeneo katika hatari ya janga la Covid-19.