Habari

COVID-19: Visa vipya ni 404 huku wagonjwa 11 wakifariki

December 15th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAGONJWA wengine 11 wamethibitishwa kufariki kutokana na Covid-19 huku watu 404 zaidi wakipatikana na virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa huo hatari.

dadi mpya ya maambukizi inawakilisha asilimia 8.2 ya maambuzi.

Kulingana na taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, Jumanne, visa hivyo vipya vya maambukizi vilitokana na sampuli 4,878 zilizopimwa ndani ya saa 24 zilizopita.

Ongezeko la visa hivyo sasa limefikisha idadi jumla ya visa vya maambukizi ya Covid-19 nchini kuwa 92,459 tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa huo kilipogunduliwa nchini mnamo Machi 13, 2020.

“Na idadi jumla ya vifo vilivyosababishwa na virusi vya corona sasa ni 1,604 baada ya wagonjwa hao 11 kuaga dunia,” akasema Bw Kagwe.

Waziri huyo pia ametangaza kuwa jumla ya wagonjwa 527 wamepona na wakaruhusiwa kurejelea maisha yao ya kawaida ambapo 408 kati yao walikuwa wakihudumiwa chini ya mpango wa uuguzi nyumbani ilhali 119 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini wakipokea matibabu.

Kwa mara nyingine Kaunti ya Nairobi imeongoza kwa kuandikisha idadi kubwa ya visa ikiwa na 118 ikifuatwa na Kilifi iliyonakili visa vipya 110.

Kaunti ya Mombasa imeandikisha visa vipya 66, Makueni (26), Nakuru (23), Kiambu (12), Kisumu (11), Turkana (9), Kwale (5), Nyeri (5), Siaya (4) , Kajiado (4), Murang’a (3) na Machakos visa viwili (2).

Nazo kaunti za Meru, Kakamega, Kericho, Kirinyaga, Marsabit na Lamu zimenakili kisa kimoja kila moja.