Habari Mseto

Covid-19: Visa vyafika 1214

May 25th, 2020 1 min read

NA BERNADINE MUTANU

Kenya imerekodi visa vingine 22 vya watu walioambukizwa virusi vya corona huku idadi ya wanaougua ikifikia watu 1214.

Akihutubia wanahabari katika jumba la Afya House, Nairobi, waziri msaidizi wa Afya Rashid Aman alisema kuwa  watu hao wana umri wa kati ya miaka 24 na 73. 17 ni wanaume na 5 ni wanawake.

“Nairobi ina visa 10, Mombasa 9, kaunti za Kwale, Nakuru na Taita Taveta zina kisa kimoja.”

Kati ya watu 10 walioambukizwa Nairobi, wawili ni kutoka mtaa wa Mathare, wawili Kibra huku Makadara, Embakasi West, Eastleigh, Ruaraka, Langata na Westlands ikirekodi kisa kimoja.

Huko Mombasa, Mvita ina visa 5, Changamwe, Likoni, Jomvu na Nyali zikiwa na kisa kimoja.

Dkt Aman alisema habari za kutia moyo ni kwamba watu watatu zaidi wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumbani huku idadi ya waliopona ikifikia watu 383.

Alisema kuwa mtu mmoja aliyeugua corona aliaga dunia akipata matibabu katika hospitali ya Mathare, huku idadi ya waliofariki ikifikia watu 51.

Aliwahimiza wananchi kujitokeza ili kupimwa huku akisema kua serikali itangaramia matitabu na karantini.

Tafsiri: Faustine Ngila