Habari

COVID-19: Wagonjwa 14 wafariki Kenya idadi jumla ya walioaga dunia ikifika 1,545

December 9th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WAGONJWA 14 zaidi walifariki Jumanne kutokana na Covid-19, siku moja baada ya idadi ya vifo kutokana na ugonjwa huo kupungua kwa kiwango kikubwa.

Mnamo Jumatatu ni wagonjwa watano pekee waliothibitishwa kufariki hali iliyoleta matumaini ya kupungua kwa maafa hayo haswa wakati huu ambapo msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya unaanza.

Lakini Jumanne, Desemba 8, 2020, Waziri Msaidizi wa Afya Mercy Mwangangi alitangaza kuwa watu 14 walifariki, na kupandisha idadi jumla ya maafa kutokana na Covid-19 kuwa 1,545.

Kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya Wizara ya Afya, jumba la Afya, Nairobi, Dkt Mwangangi pia alitangaza kuwa watu wengine 521 wapya walipatikana na virusi vya corona.

“Maambukizi hayo mapya yalipatikana baaada ya sampuli kutoka kwa watu 4,721 kupimwa ndani ya saa 24. Idadi hii imefikisha 89,100 idadi jumla ya maambukizi nchini tangu kisa cha kwanza kilipogunduliwa mnamo Machi 13,” akasema Dkt Mwangangi.

“Hata hivyo, tumeweza kupambana na ugonjwa huu kikamilifu. Hii ni kupitia Wakenya kuhakikisha kuwa wamezingatia masharti ya Wizara ya Afya ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona,” Waziri huyo Msaidizi akaongeza.

Dkt Mwangangi aliongeza kuwa wagonjwa 425 walipona na kuhurusiwa kurejelea maisha yao ya kawaida, miongoni mwao wakiwa wagonjwa 330 waliokuwa wakiuguzwa chini ya mpango wa kuhudumiwa nyumbani.

Hayo yanajiri wakati ambapo kuna hofu nchini kwamba huenda juhudi za kupambana na ugonjwa huo nchini huenda zikalemazwa na mgomo wa wahudumu wa afya ulioanza Jumatatu.

Wahudumu hao wanalalamikia uhaba wa vifaa kinga (PPE), mishahara na marupurupu finyu, ukosefu wa bima ya afya miongoni mwa matakwa mengine.

Jumanne, Dkt Mwangangi alisema serikali kuu na zile za kaunti ziko mbioni kushughulikia matakwa hayo huku akiwaomba wahudumu hao kurejea kazini.

Madaktari nao, ambao walisimamisha mgomo wao Jumatatu kutoka nafasi kwa mazungumzo kati ya viongozi wa chama chao (KMPDU) na kamati za bunge, walisema watasusia kazi kuanzia Desemba 21, 2020, ikiwa matakwa yao hayatakuwa yameshughulikiwa.

Kufikia sasa jumla ya madaktari 13 wamefariki – kufikia Jumatatu – pamoja na wahudumu wa afya katika vitengo vingine. Daktari wa hivi punde kufariki ni Stephen Mogusu aliyekata roho Jumatatu baada ya kulazwa katika chumba cha kuwahudumia wagonjwa mahututi kwa siku nne.