Habari

COVID-19: Wagonjwa 14 wathibitishwa kufariki Kenya idadi jumla ya walioangamia ikifika 1,131

November 22nd, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAGONJWA 14 zaidi walithibitishwa kufariki Jumapili kutokana na Covid-19 na hivyo kufikisha idadi jumla ya waliofariki kuwa 1, 131 tangu ugonjwa huo uliporipotiwa kwa mara ya kwanza nchini Machi 13, 2020.

Kwenye taarifa iliyotumwa na Wizara ya Afya kwa vyombo vya habari, Waziri Mutahi Kagwe alisema watu wengine 968 walithibitishwa kuwa na virusi vya corona baada ya sampuli kutoka watu 6,610 kupimwa ndani ya muda wa saa 24.

Hii inafikisha idadi jumla ya visa vya maambukizi nchini kuwa 77,372.

Waziri Kagwe pia alitangaza kuwa jumla ya wagonjwa 155 walithibitishwa kupona na kuruhusiwa kurejelea maisha yao ya kawaida.

“Watu 110 kati yao walikuwa wakitunzwa nyumbani ilhali 45 walikuwa wakipokea matibabu katika hospitali mbalimbali nchini. Kupona kwao kunafikisha 51,507 idadi jumla ya wagonjwa waliopona kufikia leo (Jumapili),” akaeleza.

Bw Kagwe aliongeza kuwa wakati huu jumla ya wagonjwa 1,131 wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini huku 7,023 wakiuguzwa nyumbani walikotengwa.

“Na wagonjwa 63 wako katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi, 36 wakisaidiwa kupumua na “ventilators” huku 26 wakiongezewa oksijeni ya ziada,” akaeleza.

Kwa mara nyingine kaunti ya Nairobi inaongozwa kwa kuandikisha visa vingi vipya vya maambukizi vikiwa 421 ikifuatwa na Mombasa yenye visa 91 kisha Kilifi yenye visa 88.

Kaunti ya Busia ina visa 73, Kiambu (54), Kajiado (30), Nakuru (22), Uasin Gishu (21), Machakos (17), Murang’a (16), Nyeri (16), Bungoma (14), Kirinyaga (13), nayo Makueni ikaandikisaha visa 11 vipya.

Kaunti za Kisumu, Turkana, Tharaka Nithi na Meru ziliandikisha visa 11 kila moja, Marsabit (8), Laikipia (4), Narok (4), Kisii (3), Homa Bay (3), Elgeyo-Marakwet (3), Mandera (3), Nandi (2), Kwale (2) huku kaunti za Kericho, Garissa, Wajir, Nyandarua na Trans-Nzoia zikiwa na kisa kimoja kila moja.