Habari Mseto

COVID-19: Wagonjwa wengine 16 wafariki wakati visa 644 vipya vikithibitishwa

December 11th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAGONJWA 16 zaidi wamefariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 huku wagonjwa 994 wakiwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini.

Kwenye taarifa iliyotumwa Alhamisi kwa vyombo vya habari, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema visa 644 zaidi vya maambukizi vilithibitishwa nchini.

Bw Kagwe pia aliongeza kuwa wagonjwa 1,060 walipona na kuongeza idadi ya wale aliopona kufikia Alhamisi kuwa 71,254.

“Ongezeko la visa vipya 644 limepandisha idadi jumla ya visa hivyo kuwa 90,305 huku idadi jumla ya waliofariki kufikia 1,568 baada ya wagonjwa 16 zaidi kuangamia,” waziri huyo akaeleza kwenye taarifa hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari.

Kwa mara nyingine Nairobi inaongoza kwa visa vipya vya maambukizi kwa kuandikisha viaa 158 ikifuatwa na kaunti jirani ya Kiambu yenye visa 69.

Kaunti ya Mombasa inashikilia nambari tatu kwa kusajili visa 67, Murang’a (56), Taita Taveta (36), Nakuru (31), Meru (26), Bungoma (19) na Busia (17).

Nayo kaunti ya Kakamega Alhamisi ilirekodi visa vipya 15 vya maambukizi ya corona, Makueni (13), Uasin Gishu (12), Tharaka Nithi (11), Kericho (11), Kilifi (10), Lamu na Kajiado visa 9, Kitui (7), Isiolo (5), Machakos (5) huku Kisumu ikinakili visa vitano vya maambukizi ya Covid-19.

Waziri Kagwe alisema kuwa miongoni mwa wagonjwa 1,060 waliopona, 910 kati yao walikuwa wakihudumiwa nyumbani ilhali 150 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini.

Bw Kagwe aliongeza kuwa miongoni mwa wagonjwa wa corona waliolazwa hospitalini, 55 wako katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa wahututi (ICU) ilhali 27 wamewekewa vifaa vya kuwasaidia kupumua.