Habari

COVID-19: Wahudumu wa afya wagoma Lamu kwa kukosa PPE

July 16th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

WAHUDUMU wa Afya wa hospitali ya rufaa ya King Fahad mjini Lamu wamegoma baada ya wenzao sita, ikiwemo madaktari na wauguzi kupatikana wakiugua maradhi ya Covid-19.

Malalamiko yao yanahusu kukosekana kwa vifaa-nyenzo hospitalini humo.

Wahudumu hao wa afya wamekuwa wakiilalamikia serikali ya Kaunti ya Lamu kwa kukosa kuwajibikia suala la vifaa vya kujikinga – PPE – dhidi ya corona.

Wale ambao tayari wamepatikana wakiugua maradhi hayo wamejiweka karantini kwenye nyumba zao.

Katika mahojiano na Taifa Leo, wahudumu hao wa afya waliogoma waliikashifu serikali ya kaunti ya Lamu kwa kukosa kujitokeza kueleza ni njia gani zifaazo za kuchukuliwa ili kuzuia maradhi hayo yasisambae zaidi hospitalini na Lamu kwa jumla.

Mmoja wa wahudumu wa afya aliilalamikia serikali ya kaunti kwa kuwatelekeza katika suala zima la Covid-19 wakiwa kazini.

“Tunaishinikiza serikali ya kaunti kuwajibikia hali yetu ya utendakazi hapa hospitalini ili sisi, wagonjwa, familia zetu na jamii nzima kuwa salama dhidi ya Covid-19,” amesema mmoja wa wahudumu hao wa afya.

Kwa kuchunguza tu, Taifa Leo imebaini kuwa ni mhudumu mmoja pekee wa afya ambaye alikuwa ameachwa kuhudumia akina mama wajawazito sehemu ya mataniti huku wengine wote wakijikusanya chini ya mwembe ndani ya hospitali hiyo ya King Fahad kusubiri kauli kutoka kwa kaunti.

Juhudi za kumpata Waziri wa Afya wa Kaunti ya Lamu, Dkt Anne Gathoni ili kuzungumzia suala hilo zimegonga mwamba kwani hakupokea simu wala kujibu jumbe alizotumiwa.

Kwa upande wake aidha, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia ambaye ni mwenyekiti wa jopo la kushughulikia Covid-19 eneo la Lamu, amethibitisha kuwa ni kweli wahudumu sita wa afya katika hospitali ya King Fahad walikuwa wakiugua maradhi ya Covid-19.

Amesema wahudumu hao wa afya waliambukizwa maradhi hayo walipokuwa kwenye harakati za kumtibu nyanya aliyefariki aliyefariki kutokana na Covid-19 akiwa na umri wa miaka 60 kwenye hospitali hiyo ya King Fahad hivi majuzi.

“Kwa sasa tuko na jumla ya visa 19 vya corona na kifo kimoja eneo hili la Lamu. Ni kweli. Kuna wahudumu sita wa afya waliopatikana na Korona kwenye hospitali ya King Fahad hivi majuzi. Walikuwa wakimtibu mama aliyefariki kwa Covid-19 hospitalini humo hivi majuzi,” amesema Bw Macharia.