Habari

COVID-19: Wakazi wa Kiambu kupimwa baada ya visa viwili kuthibitishwa Makongeni

May 17th, 2020 2 min read

LAWRENCE ONGARO na SAMMY WAWERU

GAVANA wa Kiambu Dkt James Nyoro amesema wakazi wa Kiambu wataanza kupimwa Covid-19 kwa wingi kufuatia watu wawili kugundulika wana ugonjwa huo Makongeni, Thika.

Hatua hii yake aliyoiweka wazi Jumamosi inafuatia tangazo la Ijumaa kutoka Wizara ya Afya.

Akihutubia wanahabari Ijumaa wiki jana katika makao makuu ya Wizara ya Afya, Nairobi, Waziri Msaidizi katika wizara Dkt Rashid Aman alitangaza kwamba Thika iliyoko Kaunti ya Kiambu, imekuwa ‘mwenyeji’ wa Covid-19.

Waziri alifafanua kuwa visa hivyo vilithibitishwa Makongeni Phase 4 na 5.

Habari hizo ziliibua hisia tofauti na wakazi wa eneo hilo ambapo baadhi walielezea waziwazi wasiwasi wao.

“Tuna wasiwasi baada ya visa vya Covid-19 kuthibitishwa Makongeni,” Susan Wanjiru, mkazi wa Makongeni Phase 10 akasema jana Jumamosi.

Anne Mwangi, alipokea tangazo hilo kwa uzito, akisema ni bayana shughuli za biashara kuathirika kwa kiasi kikuu.

“Wateja wameanza kupungua na kuongeza mahangaiko kwa changamoto tulizokuwa nazo awali,” mama huyo anayeuza nafaka akalalama.

Sasa Gavana Nyoro amesema watashirikiana na maafisa wa afya ili kufanikisha shughuli na mchakato wa kuwapima wakazi.

“Tunataka kuhakikisha kila kitu kinafanyika kwa utaratibu unaostahili,” akasema Dkt Nyoro akihutubu jana Jumamosi.

Kulingana na ilani iliyotolewa ni kwamba soko kuu la Madaraka liloko Makongeni mjini Thika litafungwa kwa muda ili dawa inyunyuzwe hapo kupunguza na kuua viini vya aina yoyote.

Alisema maafisa wa afya ya umma watafanya juhudi kuona ya kwamba masoko yote ya umma na sehemu za mikusanyiko ya watu zinanyunyizwa dawa.

Maafisa wa afya walisema watalifunga soko hilo kwa muda ili dawa ipulizwe kwanza kabla ya kurejelewa tena kwa shughuli zilizozoeleka.

Aidha, patawekwa kizuizi ili mpangilio mzuri uwepo wa watu kuingia ndani.

Dkt Nyoro alisema chombo maalum kitatundikwa katika soko hilo ili kila mmoja anayeingia apate sanitaiza.

Watu wote wanaouza chakula katika soko hilo wamehimizwa kuzingatia usafi wakati wote wakiwa hapo.

Hili ni soko kuu la Madaraka, Makongeni mjini Thika baada ya kufungwa kwa muda mnamo Jumamosi, Mei 16, 2020. Picha/ Lawrence Ongaro

Alitoa mwito kwa wachuuzi wanaouza chakula wadumishe usafi ili waweze kupambana na Covid-19.

“Iwapo kila mmoja atazingatia usafi na kufuata maagizo yote yaliyowekwa bila shaka tutaweza kupunguza makali ya corona kwa kiwango kikubwa,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema watafanya juhudi kuona ya kwamba wanazingatia mipaka yao ya kuingia na kutoka Kiambu ili kuzuia corona.

Alitoa mwito kwa wakazi wa Kiambu wakubali kushirikiana na maafisa hao wa afya ili kufanikisha mchakato huo.

Alisema maafisa wa afya watazuru Soko Mjinga ambalo ni soko lililoko baina ya mpaka wa Nyandarua na Kiambu kwa lengo la kupima wakazi wa eneo hilo.

“Tunataka kuweka mipaka yetu katika hali ya tahadhari ili kukabiliana na janga hili. Kwa hivyo, tunatoa pia mwito kwa wananchi wafanye jambo la busara washirikiane nasi kama serikali ili tuangamize janga linalotukabili,” alisema Dkt Nyoro.

Baadhi ya wakazi Makongeni wanataka wenye nyumba watahadhari ili watu wanaoingia kutoka kwingineko wawe wamebainika hali zao kiafya.

“Wenye nyumba za kukodisha hawajali nani anaingia katika nyumba au ploti wakati huu na hili ni hatari kwetu,” John Muya akateta.

Kufikia Jumamosi, Kenya ilikuwa na idadi jumla ya visa 830 vya waliogundulika kuwa na Covid-19 tangu kisa cha kwanza kiripotiwe Machi 13, 2020.

Kaunti ya Nairobi na Mombasa zingali zinaongoza katika idadi ya visa vya maambukizi.