Habari Mseto

COVID-19: Walemavu Thika walalama chakula cha msaada hakiwafikii

May 6th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

UGAWAJI wa chakula unastahili kuendeshwa kwa uwazi bila ubaguzi.

Walemavu na vipofu kutoka kijiji cha Kiandutu mjini Thika, wamelalamika kuwa wengi wao hawafikiwi na chakula hicho huku wakiachwa na njaa.

Wamezidi kulalamika kwamba watu wanaopewa majukumu ya kusambaza chakula hicho wana mapendeleo fulani huku wakiwajali jamaa zao na marafiki wao.

Bi Jecinta Syumbua ambaye ni mmoja wa wasiojiweza anasema wanapitia masaibu mengi ambapo wanaiomba afisi ya naibu kamishna Bw Douglas Mutai, kuingilia kati ili kuweka kamati inavyostahili kusambaza chakula hicho kwa uwazi.

Alisema hivi majuzi chakula kilipoletwa katika kijiji hicho walemavu wengi na vipofu waliachwa hoi huku watu waking’ang’ania chakula hicho.

Alisema jambo linalowakera zaidi ni kwamba wale wanaosambaza chakula hicho wamezoea kurusha hewani ili umati uweze kudaka lakini kitendo hicho hakiwafai waliolemaa kimaumbile.

Alisema kwa muda wa wiki mbili hivi wamelemewa na makali ya njaa, familia zao nyingi nazo zikikosa chakula.

Bw George Mwangu ambaye pia ni mkazi wa kijiji hicho anasema wameshindwa jinsi watakavyopata chakula kwa njia ya utaratibu kwa sababu wakati mwingi watu hung’ang’ania kwa fujo.

“Sisi kama wakazi wa hapa tunataka utaratibu mwafaka ufuatwe ili chakula kisambazwe kwa uwazi na uwajibikaji,” alisema Bw Mwangu.

Alipendekeza wanaosambaza chakula hicho washirikiane na machifu na wazee wa kijiji ili kuwe na mpangilio maalum baada ya kuandika majina ya kila mmoja anayestahili kupata chakula hicho.

Alisema iwapo mtindo huo utafuatwa kwa uwazi bila shaka kila mmoja atapata kitu cha kuweka tumboni.

“Kile kimeturegesha nyuma ni ubaguzi wa wazi kwani unaona wazi asiyestahili kupata ndiyo anapokea msaada huo wa chakula. Kwa hivyo serikali ije na mikakati kabambe itakayonufaisha wanaostahili.,” alisema Bw Mwangu.

Alisema cha muhimu pia ni kuona ya kwamba hali ya usalama inaimarishwa ili mambo iende shwari wakati wa kusambaza chakula hicho.

Wakazi hao pia walisema watu wengi katika kijiji hicho wanahitaji chakula ambapo idadi kamili inazidi watu 20,000.

Hata hivyo, wiki iliyopita Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema amepata malalamiko mengi kutoka kwa wakazi kuwa chakula cha msaada hua hakiwafikii wakazi hao jinsi inavyostahili.

“Nitahakikisha majina yote ya wanaostastahili kupewa chakula orodha inapitishwa afisini mwangu ili yakaguliwe kwanza,” alinukuliwa akisema alipozuru kijiji hicho.

Alisema mpangilio maalum utafanywa ili angalau kila mmoja apate chakula kwa sababu “kuna chakula cha kutosha.”