Habari

COVID-19: Wanahabari waitaka serikali itafute mbinu ya kutoa habari bila kuitisha vikao vinavyohatarisha afya zao

March 19th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

BARAZA la Vyombo vya Habari (MCK) limeitaka serikali ya kitaifa kutuma habari kuhusu matukio ya maambukizi ya virusi vya corona kwa vyombo vya habari.

Kulingana na maagizo hayo mapya, kitengo cha MCK kuhusu masuala ya dharura kinaitaka ofisi ya msemaji wa serikali na idara za mawasiliano katika serikali za kaunti kusitisha mtindo wa kuwaita wanahabari kuwahutubia ili kuzuia mikusanyiko ya wanahabari na hivyo kuhatarisha maisha yao.

MCK inasema kuwa ili wanahabari waweze kuzingatia mwongozo uliotolewa na Wizara ya Afya kuhusu njia za kujikinga dhidi ya maambukizi ya Covid-19, hawafai kuruhusiwa kukongama.

Vyumba vya habari, ikaongeza, vinafaa kuupa kipaumbele usalama wa wanahabari, MCK ikasema kwenye taarifa.

“Serikali ya Kitaifa, Serikali za Kaunti, Mashirika na Sekta Binafsi zinapaswa kusitisha vikao vyote na wanahabari ili kuzingatia maagizo yaliyotolewa na Wizara ya Afya ya kuzuia maambukizi ya Covid-19,” ikasema MCK.

Ikaongeza: “Serikali ya Kitaifa inapasa kuhakikisha kuwa imetoa habari za moja kwa moja kwa vyombo vya habari katika ngazi zote. Hii itahakikisha kuwa masharti ya wizara ya afya ya kuepuka kusongamana yanazingatiwa.”

Hata hivyo, baraza hilo liliongeza kuwa endapo wanahabari wanahitaji kufuatilia habari muhimu kwa kukutana na maafisa wa serikali, basi sharti wapewe vifaa vya kujikinga.

Kufikia sasa serikali imethibitisha visa saba vya maambukizi ya virusi vya corona nchini.

Janga hilo limesababisha vifo vya zaidi ya watu 8,800 kote duniani kutoka kwa idadi jumla ya watu 220,000 walioambukizwa.

Na jumla ya watu 84,000 kote duniani wamepona kutokana na ugonjwa huo unaojulikana kama Covid-19.