Habari

COVID-19: Wanaharakati walaani hatua ya polisi kuwakamata waandamanaji saba Mombasa

August 25th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

WAANDAMANAJI saba kutoka mashirika tofauti ya kutetea haki za kibinadamu katika Kaunti ya Mombasa wamekamatwa na maafisa wa polisi Jumanne asubuhi walipokuwa katika maandamano wakitaka waporaji wa fedha za kupambana na janga la corona wakamatwe.

Waandamanaji hao wameanza shughuli zao katika eneo la Pembe za Ndovu, katikati mwa jiji la Mombasa na walipofika eneo la Posta, wametawanywa kwa vitoa machozi huku wengine wakikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Central.

Maafisa wa polisi wamewatawanya wakidai kuwa walivunja sheria ya kutotangamana iliyowekwa na Wizara ya Afya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Baadhi ya waliokamatwa ni mwanaharakati Francis Auma kutoka shirika la kutetea haki za kibinadamu (Muhuri) na mwenzake Lucas Fondo.

Pia baadhi ya wanafunzi kutoka vyuo vikuu kadhaa wamekamatwa.

Wakizungumza nje ya kituo hicho cha polisi, viongozi wa mashirika mbalimbali ya kutetea haki wamedai kuwa maafisa hao wa polisi wamekiuka sheria kwa kuwakamata wanaharakati hao waliokuwa wakifanya maandamano kwa amani.

Mkurugenzi wa shirika la Haki Yetu, Padre Gabriel Dolan amedai serikali haitaki Wakenya waandamane kupinga ufisadi unaoendelea, haswa katika Wizara ya Afya.

“Wanawakamata watu wadogo na wanyonge kama sisi badala ya kuwakamata na kuwafunga viongozi wafisadi katika serikali,” amesema Padre Dolan.

Amesema Wakenya hawawezi kusahau maovu yanayoendelea “hata wakijaribu kutunyamazisha, tutazungumza kwa kuwa wakiiba fedha hizo, wanamwangamiza Mkenya ambaye anazihitaji.”

Mwenyekiti wa Muhuri, Khelef Khalifa amewahimiza Wakenya wote wazalendo waungane kupinga ufisadi.

Mwenyekiti wa shirika la kutetea haki za binadamu la Muhuri, Khelef Khalifa akizungumza na waandishi wa habari nje ya kituo cha polisi cha Central, Mombasa, Agosti 25, 2020. Amewasihi Wakenya wazalendo wajitokeze kupinga ufisadi unaoendelea serikalini. Picha/ Diana Mutheu

“Viongozi wetu wanazidi kutufeli na sasa ni wakati wa Wakenya wote wazalendo kuungana na kukashifu ufisadi unaoendelea humu nchini,” akasema Bw Khelef.

Mwanaharakati kutoka shirika liitwalo Kituo cha Sheria, Bw Zedekiah Adika amesikitika kuwa baadhi ya wanaharakati waliokamatwa walipigwa na kuumizwa walipofikishwa katika kituo cha polisi cha Central.

“Kwanza, tunaomba tuelezwe ni kwa nini wenzetu wamekamatwa na walioumizwa wanafaa wafikishwe hospitalini watibiwe. Kuandamana ni haki yetu na waliokamatwa sharti waachiliwe,” amesema Bw Adika.

Waandamanaji hawa wamebeba mabango na kuimba nyimbo huku sauti zikisikika “shika wezi”.

Wametishia kuwa hawatashurutishwa na maafisa wa polisi na kwamba maandamano yataendelea hadi pale waliohusika katika kashfa ya wizi wa fedha zilizotengwa kupambana na janga la corona, watakamatwa.

Maandamano kama hayo pia yalifanyika katika kaunti za Kisumu, Nakuru na Nairobi.