Habari Mseto

COVID-19: Wananchi wafurika masokoni kununua vyakula

March 27th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MASOKO ya bidhaa za kula eneobunge la Ruiru yalishuhudia idadi kubwa ya watu kufuatia notisi iliyotolewa ikiyataka yasitishe shughuli zake za biashara kufikia mwishoni mwa jana Alhamisi, Machi 26, 2020.

Mkuu wa kaunti ndogo ya Ruiru, Stephen Kiiru, kwenye barua kwa wakuu wa masoko hayo na vibanda vilivyoko kandokando mwa barabara, pamoja na wachuuzi, aliamuru yafungwe kwa muda wa siku 21 ili kudhibiti maenezi zaidi ya Covid-19.

Yaliyotajwa ni pamoja na soko la Ruiru Mjini, masoko ya Githurai ndiyo Jubilee na Migingo.

Alhamisi masoko ya bidhaa za kula, watu walifurika, katika harakati za lala salama kujihami kwa bidhaa za kutosha ikizingatiwa kuwa hali ya janga la virusi hatari vya Corona haijulikani itakavyokuwa.

Wauzaji wa nafaka, mahindi mabichi, maboga, viazi, mboga, vitunguu, nyanya, miongoni mwa bidhaa zingine za kula walishuhudia idadi kubwa ya wateja.

“Kuanzia Jumatano, watu wamekuwa wakinunua bidhaa za kula kwa wingi,” muuzaji wa vitunguu aliyejitambulisha Mama Njambi akaambia ‘Taifa Leo‘.

Serikali ya kaunti ya Kiambu pia imeamuru masoko yote humo yafungwe. Ni hatua ambayo imetia wengi kiwewe, wakihofia kwa muda wa siku 21 zijazo kuanzia Machi 26 watakosa mahala pa kununua bidhaa za kula.

“Hatuna budi ila kununua vyakula kwa wingi, tuviweke kama akiba. Janga la Covid-19 halijulikani litachukua muda kiasi gani. Tumeona mataifa yaliyoathirika pakubwa kafyu ikitolewa,” akasema mnunuzi.

Kwa wafanyabiashara, hasa mazao ya kilimo, walieleza hofu ya stoki ya bidhaa zao kuoza endapo hazitanunuliwa kuisha.

“Tunalazimika kuuza kwa bei nafuu ili kukwepa hasara zaidi. Bidhaa zitakazosalia zitaozea kwenye maghala,” akalalamika mfanyabiashara muuzaji wa viazi.

Maeneo yanayokongamana idadi kubwa ya watu, kama vile makanisa, mabaa na ya burudani, serikali imeyapiga marufuku ili kuzuia maambukizi na maenezi zaidi ya maradhi ya Covid-19.

Kufikia sasa Kenya imethibitisha visa 31 vya wagonjwa walioambukizwa virusi hivyo hatari vya corona, mmoja kati yao akiripotiwa kupona kabisa.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe akitangaza Alhamisi kwamba mmoja alifariki kutokana na Covid-19 lakini akaongeza kwamba mhanga aliyekuwa na umri wa miaka 66 alikuwa na kisukari.

Rais Uhuru Kenyatta Jumatano alitangaza kafyu kati ya saa moja za jioni hadi saa kumi na moja asubuhi itakayoanza leo Ijumaa, Machi 27, 2020.

Wachanganuzi wa masuala ya kiuchumi wanahoji kufungwa kwa masoko ni hatua itakayosababisha hali ngumu ya maisha, hasa kwa mwananchi wa kawaida, mwenye mapato ya chini na kadri, ikiwa ni pamoja na kudorora kwa uchumi.