Habari Mseto

Covid-19: Watu wengi zaidi wapona

June 4th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KENYA Jumatano iliandikisha idadi kubwa zaidi ya watu 54 waliopona Covid-19 huku idadi ya watu walioambukizwa ikipanda hadi 2,126.

Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman jana alisema kupona kwa wagonjwa hao sasa kunafikisha jumla ya waliopona kufikia 553 tangu ugonjwa huo ulipogunduliwa nchini Machi mwaka huu.

“Hii ni idadi ya juu zaidi ya wagonjwa walipona na kuruhusiwa kwenda nyumbani ndani ya saa 24 zilizopita. Ni thibitisho kwamba ugonjwa huu unaweza kutibiwa na sio hukumu ya kifo; na nawapongeza wahudumu wetu wa afya kwa kazi nzuri,” akasema.

“Lakini ningependa kukariri umuhimu wa kila mmoja wetu kuendelea kuzingatia masharti ya kuzuia maambukiza ya virusi vya corona kama vile kuvalia barakoa na kutotangama,” Dkt Aman akaongeza jana alipotoa taarifa ya kila siku kuhusu janga hilo jijini Nairobi.

Alitangaza kati ya sampuli  2,112 za watu waliopimwa 123 zilithibitishwa kuwa na virusi vya corona. Jumla ya sampuli ambazi zimepimwa kufikia jana sasa ikifikia 85,058.

Na watu watatu zaidi walifariki kutokana na Covid-19 na hivyo kufikisha 74 idadi ya maafa kufikia jana.

Kwa mara nyingine Nairobi iliongoza kwa kuwa na watu 44 wapya waliothibitishwa kuwa na virusi vya corona ikifuatwa na kaunti ya Mombasa iliyokuwa na watu 34.

Kaunti zingine zilikopatikana  visa vya maambukizi mapya ya virusi vya corona jana ni; Busia (visa 20), Uasin Gishu (12), Kajiado (3), Kiambu (3), Nyeri (3), Kilifi (2) huku Garissa na Laikipia zikiwa na kisa kimoja kila moja.

Katika kaunti ya Nairobi eneo bunge la Kibra liliongoza kwa visa 10, Westlands (9), Dagoreti (4), Embakasi Magharibi (4), Embakasi Kusini (3), Langat (3), Makadara (3), Kasarani (3) huku Ruaraka na Kamukunji zikiwa na mgonjwa mmoja kila moja.

Eneo Bunge la Mvita linaongoza katika kaunti ya Mombasa kwa visa 11, Jomvu (8), Likoni (4), Kisauni (3) na Nyali (3).