Habari Mseto

COVID-19: Wizara yaonya wanasiasa wanaokiuka masharti

September 8th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine Wizara ya Afya imewaonya wanasiasa dhidi ya kukiuka masharti ya kuzuia kusambaa kwa ugonjwa hatari wa Covid-19.

Hii ni baada ya wanasiasa, wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuandaa msururu wa mikutano mwishoni mwa wiki jana ambapo waliohudhuria walionekana kutangamana na kutovalia barakoa.

“Wale ambao wanaandaa mikutano ya hadhara wanavunja sheria. Nawaonya kuwa mikutano na mikusanyiko kama hiyo ya watu inaweza kutoa mazingira faafu ya kusambaa kwa virusi vya corona,” Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman akasema.

Alikuwa akitoa taarifa kuhusu hali ya maambukizi ya Covid-19 nchini ndani ya saa 24 kufikia jana alasiri.

Mnamo Jumapili Dkt Ruto alihutubia mkutano wa hadhara eneo la Athi River baada ya kuhudhuria ibada katika Kanisa la Anglikana (ACK) la St Paul.

Picha zilizopeperushwa katika vyombo vya habari zilionyesha Naibu Rais akituhutubia umati mkubwa wa watu uliozingira msafara wake ambapo aliwakemea mawaziri wanaojiingiza katika siasa akiwataka wajiuzulu.

Alihutubia umati huo akiwa juu ya gari lake huku wananchi wakimsikiza na kumshangilia; wengi wao wakiwa hawajavalia barakoa.

Naye Bw Odinga alihutubia msururu wa mikutano ya kisiasa katika Kaunti ya Kakamega ambapo wanasiasa waliohudhuria hawakuzingatia kanuni ya kutotangamana hapa kwa maana ya kutokaribiana sana.

“Wanasiasa ambao wanaendelea kuandaa mikatano hii ya hadhara wanavunja sheria. Hatua kali itachukuliwa dhidi yao,” akawaambia wanahabari katika makao makuu ya Wizara ya Afya, Jumba la Afya, Nairobi.

Jumbe za wanasiasa kutoka sehemu mbalimbali za nchi zimekuwa zikitembelea makazi rasmi ya Dkt Ruto mtaani Karen katika kile kinachosemekana kuwa mbinu zake za kujipigia debe kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Wanasiasa wa mrengo wa handisheki pia wamefanya msururu wa mikutano nyumbani kwa Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Cotu) Francis Atwoli kujadili siasa za urithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Hii ni licha ya kwamba Wizara ya Afya ilipiga marufuku mikutano yote ya hadhara ili kuzuia msambaa wa virusi vya corona.

Janga hilo tayari limesababisha vifo vya zaidi ya watu 580 tangu kisa cha kwanza cha maambukizi kilipogunduliwa nchini Kenya mnamo Machi 13, 2020.

Mnamo Jumatatu watu 102 zaidi walipatikana na virusi hivyo huku wagonjwa wawi zaidi wakifariki.

Idadi hiyo ya maambukizi mapya ilithibitishwa baada ya sampuli 2,668 kupimwa ndani ya saa 24, hivyo kufikisha 35,205 idadi jumla ya maambukizi nchini.