Habari Mseto

Covid: Hofu ya vifo kuongezeka kaunti yatanda

November 6th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

VIONGOZI wa Kiislamu katika Kaunti ya Mombasa wamewaonya wakazi waache kukana kuwa hakuna ugonjwa wa Covid-19, kufuatia ilani kwamba baadhi ya makaburi yanakaribia kujaa kwa ongezeko la vifo.

Mwenyekiti wa kamati ya Waislamu ya kushughulikia Covid-19 katika kaunti hiyo, Bw Rajab Ramadhan, alitaka Waislamu wote wafuate kanuni za Wizara ya Afya kuepusha maambukizi.

“Jameni, tumekanywa mara nyingi na itakuwa vyema iwapo tutafuata hatua zilizowekwa na serikali, ili tujilinde,” akasema Bw Ramadhan.

Naibu Mwenyekiti wa makaburi ya Kikowani, Captain Khamis, alitahadharisha Waislamu Mombasa kwamba idadi ya vifo vilivyoshuhudiwa katika muda wa wiki moja iliyopita inatia wasiwasi.

Kulingana na Bw Khamis, katika wiki mbili zilizopita, makaburi hayo yameshuhudia kati ya mazishi matatu hadi matano kwa siku, baadhi yakihusishwa na Covid-19.

“Hivi karibuni, hakutakuwa na nafasi ya kuzika watu zaidi katika makaburi hayo,” akaonya.

Imam wa Msikiti wa Spaki, Abu Hamza alisema mikutano ya mazishi inapaswa kuepukwa kwani Waislamu wengi wameambukizwa maradhi hayo baada ya kuhudhuria mikutano ya kupanga mazishi bila kujali.

“Tunawasihi Waislamu wote waache kuhudhuria mikutano ya mazishi kwani wanaambukizana virusi hivyo kwenye mikusanyiko hiyo, na bila tahadhari, ugonjwa huu utatumaliza,” alisema Imam Hamza.

Wakati huo huo, maambukizi Alhamisi yaliendelea kuripotiwa shuleni.

Shule ya Upili ya Bahati, Kaunti ya Nakuru ilifungwa kwa muda baada ya wanafunzi 68, walimu watano na wafanyikazi wawili kupatikana na ugonjwa wa Covid-19.

Kwenye taarifa ya waziri wa afya wa kaunti, Dkt Kariuki Gichuki, alisema matokeo ya vipimo yalitambulika Jumatano jioni baada ya sampuli kuchukuliwa mapema juma hili.

“Shule hiyo sasa ni eneo la kutenga wagonjwa wa Covid-19 ili kudhibiti maambukizi zaidi,” akasema.

Alieleza kuwa wanafunzi 115 wako kwenye karantini na maafisa wa afya wanazidi kufuatilia hali yao.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi Catherine Wangare alisema idadi ya jumla ya wanafunzi wa kidato cha nne ni 183.

Mwanafunzi mmoja kati ya walioathirika alilemewa na kukimbizwa katika hospitali ya Nakuru ambapo anaendelea na matibabu.

Afisa mkuu wa idara ya umma Bw Samuel King’ori alisema hali ya mwanafunzi huyo iko imara na wazazi wake wamearifiwa ipasavyo.

Na katika shule ya wavulana ya Kolanya, maafisa walisema imegeuzwa kuwa eneo la kutenga wagonjwa baada ya wanafunzi 52 kuripotiwa kuambukizwa ugonjwa huo mapema wiki hii.

Walimu sita na wafanyakazi wawili pia wameambukizwa.

Walioathirika wametengwa huku wanafunzi wengine wakizuiliwa katika bweni ambapo wahudumu wa afya wanashughulikia hali yao. Hata hivyo, wanaendelea na masomo katika sehemu hizo.

Walimu na wafanyikazi walioathirika katika shule hizo wametengwa manyumbani mwao ambapo wanaendelea kudhibiti hali hiyo.

Mkuu wa elimu katika kaunti ya Teso Bw Naftali Ombati alisema tayari maafisa wa afya wanadhibiti hali ya wanafunzi na kwamba hawataruhusiwa kwenda nyumbani.

Ripoti Za Diana Mutheu, Phyllis Musasia Na Brian Ojamaa