Habari Mseto

Covid: KPA yapunguza shughuli

November 6th, 2020 1 min read

Na ANTHONY KITIMO

MAMLAKA ya Bandari Nchini (KPA) imepunguza shughuli katika vituo vyake vyote na kuweka masharti zaidi ili kuwakinga wafanyakazi wake dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Hii ni kufuatia ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo nchini.

Wafanyakazi ambao hawahudumu katika idara zenye umuhimu mkubwa, wenye umri wa miaka 58 kwenda juu na wale wenye matatizo ya kiafya wameagizwa kufanya kazi kutoka nyumbani.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Salim Rashid pia amesitisha mikutano yote ambao wafanyakazi hufanya nje isipokuwa ile ambayo imeidhinishwa na mamaneja wakuu.

KPA pia imewataka wateja wake kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao kupunguza mwenendo wa matumizi ya karatasi huku watu wanaofika katika afisi zake wakishauriwa kuzingatia masharti ya kuzuia maambukizi ya Covid-19.

Idadi ya watu wanaoambukizwa virusi vya corona nchini inaendelea kuongezeka katika maeneo mengi ya nchi.