Covid: Sakata ya uuzaji wa vyeti yaibuka

Covid: Sakata ya uuzaji wa vyeti yaibuka

Na AMINA WAKO

MAAFISA walaghai katika Wizara ya Afya (MoH) wanauza vyeti vya chanjo ya Covid-19 kwa Sh1,000.

Uchunguzi wa Taifa Leo umethibitisha kuwa sakata hiyo inahusisha maafisa wa MoH wakishirikiana na watu binafsi katika kuuza vyeti hivyo.Biashara hiyo imepamba moto zaidi wiki hii baada ya Serikali kutangaza kuwa karibuni Wakenya watahitajika kuonyesha cheti cha chanjo ya Covid-19 kabla ya kupokea huduma za serikali ama kusafiri kwa magari ya umma kama vile ndege na reli.

Uchunguzi wetu ulionyesha kuwa maafisa husika wa MoH wanatekeleza ukora huo kwa kupenya kwenye mtandao wa wizara wa MoH Chanjo, ambapo wanawatengenezea vyeti maelfu ya Wakenya wanaotaka kuhepa kuchanjwa.

Unachohitajika kufanya ili kupata cheti bila kuchanjwa ni kutuma Sh1,000 kwa afisa fulani katika kituo cha kutoa chanjo. Baada ya dakika tano pekee unapokea ujumbe mfupi wa simu kutoka MoH kuthibitisha kuwa umedungwa chanjo yay a Janssen ya kampuni ya Johnson & Johnson.

Wachunguzi wa ‘Taifa Leo’ walituma Sh3,000 na kutuma habari za watu ambao bado hawajachanjwa. Muda mfupi baadaye walipokea SMS kuthibitisha wamechanjwa.Watu hao tuliotumia kisha waliingia kwenye mtandao wa MoH Chanjo na kuthibitisha kuwa habari zao zilikuwa zimenakiliwa, kisha wakaweza kupata vyeti vyao humo.

Uchunguzi wetu pia umebainisha kuwa kwa Sh500 unapewa cheti cha chanjo za AstraZeneca ama Moderna.

Ulaghai

Ulaghai huu unaendelea wakati ambao Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ametangaza kuwa Wakenya wasio na vyeti vya chanjo watanyimwa vyeti katika ofisi za serikali kuanzia Desemba 21, 2021.Uchunguzi wetu pia umefahamu kuwa maafisa wa afya wanauza chanjo, hasa nchini Ethiopia kupitia mpaka wa Moyale.

Katika uchunguzi zaidi tulifaulu kununua chupa moja kwa Sh3,000.Alipoulizwa kuhusu kashfa hii, Bw Kagwe alielezea kushangaa kwake akisema mhudumu yeyote wa afya atakayepatikana amehusika atafutiwa leseni yake ya kazi.

Kuhusu uuzaji wa vyeti kwa watu ambao hawajachanjwa, Bw Kagwe alisema wizara yake itafanya uchunguzi na kuwachukulia hatua kali wahusika.Kufikia sasa ni watu wazima wapatao milioni 6.4 ambao wamechanjwa hapa Kenya.

Hii ina maana kuwa serikali itahitajika kuchanja raia waliobaki milioni 27 kufikia Desemba 21 ili kutekeleza vitisho vyake vya kuwanyima huduma.Hata hivyo, kuibuka kwa sakata ya kuuza vyeti inatishia kuzamisha juhudi za serikali kwani hata wale ambao hawajapata chanjo hiyo sasa wanaweza kupata cheti kwa kulipa Sh1,000 ama Sh500.

Mbali na kuhujumu vita dhidi ya Covid-19, sakata hii pia inatishia kuibua matatizo kwa Wakenya wanaosafiri kuenda ng’ambo, kwani vyeti vya Kenya huenda vikakataliwa na mataifa ya kigeni.

You can share this post!

Malawi yamsihi Mike Tyson awe balozi wake wa bangi

Wahanga wa ghasia za 2007 wafidiwe kabla ya Uhuru kutoka...

T L