Covid: Serikali yakana wandani wa Museveni walipewa chanjo

Covid: Serikali yakana wandani wa Museveni walipewa chanjo

Na DAILY MONITOR

KAMPALA, Uganda

IMEIBUKA wandani wa karibu wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda walipewa chanjo dhidi ya virusi vya corona, aina ya Sinopharm kutoka China, miezi kadhaa kabla ya wahudumu wa afya na makundi mengine nchini humo kufikiwa.

Ripoti hizo zilifichuliwa Alhamisi iliyopita na gazeti la The Wall Street Journal la nchini Amerika.

Kulingana na gazeti hilo, juhudi hizo ni sehemu ya serikali ya China kuitafutia soko chanjo yake, kama ilivyofanya katika nchi za Peru na Ufilipino.

Gazeti lilieleza kuwa nchini Peru, karibu watu 500 wenye ushawishi kisiasa walipewa chanjo hiyo kisiri, ijapokuwa inaendelea kufanyiwa majaribio. Miongoni mwao ni rais wa zamani, Martin Vizcarra.

Hata hivyo, Afisa Mkuu wa Mawasiliano wa Rais Museveni, Don Wanyama, alikanusha madai hayo, akisema nchi hiyo bado haijapokea chanjo dhidi ya virusi. Badala yake, alisema wahudumu wa afya ndio watakaopewa kwanza, mara tu zitakapowasili.

“Wanamaanisha nini wanaposema ‘watu wa karibu’? Hayo si kweli hata kidogo. Raia wa Uganda bado hawajapokea chanjo yoyote dhidi ya corona,” akasema Wanyama, kwenye mahojiano na gazeti la Daily Monitor Jumatano.

Akaongeza: “Rais ameeleza wazi kwamba tunatarajia kupata chanjo hizo hivi karibuni. Zitakapowasili, ishawekwa wazi kuwa wahudumu wa afya na watu walioathirika kiafya ndio watakaopewa kwanza. Hakuna kundi linaloitwa ‘washirika wa karibu’.”

Msemaji wa Wizara ya Afya, Emmanuel Ainebyoona, pia alikanusha kufahamu ripoti kama hizo.

“Hakuna lolote kama hilo,” akaeleza.

Juhudi za kuufikia Ubalozi wa China nchini humo hazikufua dafu.

Mnamo Desemba mwaka uliopita, serikali ya Uganda iliiruhusu jamii ya Liao Shen kutoka China kuingiza dozi 4,000 za chanjo hiyo nchini kwa matumizi yake binafsi. Jamii hiyo inaishi katika eneo la Kapeeka, wilaya ya Nakaseke, inakoendesha shughuli za kibiashara.

Waziri wa Afya, Ruth Jane Aceng, aliliambia gazeti hilo kuwa wakati huo, chanjo hiyo bado ilikuwa ikifanyiwa majaribio na ilikusudiwa kutumiwa na raia wa China pekee.

“Walitaka kuitumia wao wenyewe. Tuliwaagiza wahakikishe wanaitumia wao pekee, kwani hatutaki iwafikie raia wale wengine. Uganda huwa inaagiza chanjo ambazo zimeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) pekee kwa matumizi ya binadamu,” akasema.

Alipoulizwa jinsi serikali itahakikisha chanjo hiyo haitawafikia raia, waziri alisema itasafirishwa nchini kwa kiwango kidogo kidogo, na kuwasilishwa moja kwa moja kwa ubalozi wa China.

Msimamizi Mkuu wa jamii ya Liao Sheng, Zhang Hao, alisema chanjo hiyo haikuwa ikilenga kutumika kwa majaribio ya kimatibabu, lakini ya matumizi ya raia wa China pekee.

You can share this post!

Wadau walia utalii unaendelea kusambaratika nchini

TAHARIRI: Serikali iifuatilie ripoti kuhusu njaa