Covid: Uhaba wa vitanda, oksijeni waua wengi Afrika

Covid: Uhaba wa vitanda, oksijeni waua wengi Afrika

Na MASHIRIKA

BRAZAVILLE, CONGO

VIFO vinavyosababishwa na janga la corona barani Afrika vinaongezeka kwa asilimia 43 kwa wiki kutokana na uhaba wa vitanda vya kuhudumia wagonjwa mahututi na hewa ya oksijeni huku aina ya mpya ya virusi vya Delta ikiongezeka katika mataifa mengi, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema.

Vifo vinavyohusishwa na corona katika eneo la Afrika viliongezeka hadi 6,273 kuanzia Julai 5 hadi Julai 11 ikilinganishwa na 4,384 wiki iliyotangulia.

“Vifo vimekuwa vikiongezeka kwa muda wa wiki tano zilizopita. Hii ni ishara ya wazi kwamba hospitali katika nchi zilizoathirika zimelemewa,” alisema Dkt Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO barani Afrika.

“Nchi nyingi zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wahudumu wa afya, dawa, vifaa na wadi zinazohitajika kushughulikia wagonjwa mahututi wa corona,” alisema Dkt Moeti akizungumza akiwa jiji kuu la Congo Brazzaville.

WHO ilisema kwamba kuongezeka kwa vifo kunatokana na uhaba wa chanjo, kusambaa kwa aina mpya na hatari ya virusi ya Delta ambayo sasa imethibitishwa katika nchi 21 za Afrika na umma kuchoshwa na kanuni za kuzuia janga hili.

Shirika hilo limeonya kuwa aina nyingi hatari za virusi vya corona zinaweza kutokea ulimwenguni huku visa vipya 500,000 vya maambukizi vikiripotiwa kila siku hasa kutokana na virusi aina ya delta.

“Janga hili haliko karibu kuisha,” kamati ya dharura ya WHO ilisema kwenye taarifa.

Ilisema kwamba kuna uwezekano wa kuzuka na kusambazwa kwa aina hatari zaidi za corona ulimwenguni ambazo itakuwa vigumu kuangamiza.

Kulingana na wanasayansi wa Senegal, kuna hofu ya virusi aina ya Delta kubadilika kuwa mbaya zaidi na ambazo zitasambaa kwa haraka.

Bara la Afrika limethibitisha jumla ya maambukizi milioni sita ya corona, idadi ambayo ni ya chini ikilinganishwa na bara nyingine.

Wataalamu wanaonya kwamba huenda idadi kamili ya maambukizi haijabainika kutokana na ukosefu wa vipimo.

Mnamo Alhamisi, viongozi wa mataifa ya Afrika waliomba Benki ya Dunia kuwasaidia na Sh100 bilioni ili nchi zao zipate kufufua uchumi uliodorora kutokana na athari za janga la corona.

“Bado kuna mengi ya kufanya kujikwamua kutoka janga hili,” alisema Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara akifungua mkutano huo jijini Abidjan.

“Ni chini ya asilimia moja ya watu barani Afrika ambao wamepata chanjo ya kwanza ya corona, ikilinganishwa na asilimia 54 Amerika na barani Ulaya.”

Mahamat Faki, mwenyekiti wa muungano wa Afrika, aliomba afueni ya madeni kwa mataifa ya Afrika akisema yanahitaji kununua chanjo na kuweka misingi ya kufufua uchumi.

You can share this post!

Mganga ataka shirika limrejeshee Sh18.5m

TAHARIRI: Wahisani wajitolee kudhamini spoti