Covid: WHO yaelezea hofu ya virusi vipya vya Delta

Covid: WHO yaelezea hofu ya virusi vipya vya Delta

Na MASHIRIKA

BEIJING, China

ONGEZEKO la visa vya maambukizi ya virusi vipya vya corona aina ya Delta limezilazimu China na Australia kuweka masharti makali ya kuzuia msambao wake Jumamosi huku Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kuvidhibiti kabla ya kusababisha maafa zaidi.

Jumamosi, China ambayo ilikuwa imefaulu kudhibiti kabisa ugonjwa huo, ilirekodi visa kadha vya maambukizi katika mkoa wa Fujian na jiji lenye watu wengi la Chongqing.

Vile vile, zaidi ya visa 200 vipya vya maambukizi vilihusishwa na Delta katika jiji la Nanjing ambako wahudumu tisa katika uwanja mmoja wa kimataifa wa ndege walipatikana na virusi hivyo. Maambukizi mengine pia yalinakiliwa katika jiji kuu Beijing na mikoa mingine mitano, kufikia Jumamosi.

Hali hiyo imeilazima nchi ya China ambayo ndio chimbuko la ugonjwa huo kudhibiti matembezi ya zaidi ya watu milioni moja na kuanzisha upya mpango wa kuwapima watu corona kwa wingi.

Isitoshe, kwa mara nyingine visa vya maambukizi ya virusi vya corona vimeongezeka katika mataifa mbalimbali ulimwenguni huku Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ikitangaza ongezeko la kima cha asilimia 80 la maambukizi ndani ya kipindi cha majuma manne katika nchini mbalimbali.

Ongezeko hilo, WHO, inasema linachochewa na virusi aina ya Delta.

Aina hiyo ya virusi vya corona iligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini India lakini sasa imesambaa katika zaidi ya mataifa 132 ulimwenguni.

“Ujio wa Delta inatoa onyo kali; onyo kwamba virusi hivi vinabadilika kila mara. Lakini pia inatuzindua kwamba tunapaswa kuchukua hatua kabla ya aina nyingine za virusi kuchipuza,” mkurugenzi wa WHO anayesimamia majanga Michael Ryan akaaambia kikao cha wanahabari.

Alisisitiza kanuni za awali za mtu kukaa umbali wa mita moja na mwenzake, kuvalia barakoa nyakati zote maeneo ya umma, kudumisha usafi na kupata chanjo zapaswa kuendelea kuzingatiwa kuenea kwa aina hii ya virusi.

Lakini, imebainika kuwa mataifa tajiri na masikini, yanajizatiti kupambana na Delta huku mng’ang’anio wa chanjo kati yao ukishuhudiwa.

Nchini Australia, ambako asilimia 14 ya watu wote wamepewa chanjo, Jumamosi jiji la tatu kwa ukubwa Bristone liliwekewa amri ya kutotoka nje. Hii ni baada ya visa sita vya maambukizi ya virusi vya Delta kugunduliwa.

Taifa hilo pia liliendeleza mpango wa utoaji chanjo kwa makundi mbalimbali ya raia wake.

Lakini huku mataifa ya ulimwenguni yaking’ang’ania chanjo ili kushinda vita Delta, Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa (CDC) nchini Amerika Jumamosi kikitoa matokeo ya utafiti ulionyesha watu waliopewa chanjo bado wanaweza kueneza ugonjwa huo sawa na wale ambao hawajapata kinga hiyo.

Uchunguzi uliofanywa kaskazini mwa jimbo la Massachusetts uligundua kuwa asilimia 75 ya watu waliopata maambukizi mapya ni wale ambao walikwisha kupata chanjo.

Ripoti hiyo iliyotolewa Ijumaa jioni ilibaini kuwa idadi ya watu walioambukizwa tena baada ya kupewa chanjo ilipanda hadi 900.

Ni baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo ambapo utawala uliamuru watu waliopata chanjo kuanza tena kuvalia barakoa katika maeneo yenye hatari ya maambukizi.

You can share this post!

Raila anavyosuka ODM na Nyanza tayari kwa 2022

Lionesses yaridhika na nambari 10 Olimpiki raga ikitamatika