KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Croatia kwenye mizani ya wauaji Japan wanaolenga 8-bora kwa mara ya kwanza katika historia

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Croatia kwenye mizani ya wauaji Japan wanaolenga 8-bora kwa mara ya kwanza katika historia

Na MASHIRIKA

JAPAN watapania kuendeleza ubabe wa kuzamisha miamba wa dunia kwa mara nyingine watakapokutana na wanafainali wa 2018, Croatia, katika pambano la raundi ya 16-bora ugani Al Janoub, Qatar, mnamo Disemba 5, 2022.

Kikosi cha Japan kinachonolewa na Hajime Moriyasu kilimaliza kampeni za Kundi E kileleni baada ya kuaibisha Uhispania na Ujerumani katika kundi hilo lililojumuisha pia Costa Rica. Japan walianza kampeni zao kwa kupepeta Ujerumani 2-1 na kupokeza Uhispania kichapo sawa na hicho baada ya Costa Rica kuwakung’uta 1-0.

Croatia waliopigwa 4-2 na Ufaransa katika fainali ya Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, waliambulia nafasi ya pili katika Kundi F. Walitoshana nguvu na Morocco kwa sare tasa kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Ubelgiji baada ya kukomoa Canada 4-1.

Japo Croatia wanapigiwa upatu wa kushinda mechi ya leo, ufanisi wa kuangusha Uhispania na Ujerumani waliotawazwa mabingwa wa dunia 2010 na 2014 mtawalia inatarajiwa kuchangia motisha ya vijana wa Moriyasu.

Japan waliotinga hatua ya 16-bora kwenye Kombe la Dunia miaka minne iliyopita nchini Urusi, hawajawahi kufuzu kwa robo-fainali za kivumbi hicho katika historia.

Chini ya kocha Zlatko Dalic, Croatia watajibagwa ulingoni wakilenga kuendeleza rekodi ya kutopigwa katika mechi tisa zilizopita katika mashindano yote.

Tangu Japan ilime Croatia 4-3 katika mechi yao ya kwanza miaka 25 iliyopita, masogora wa Dalic walilipiza kisasi kwa ushindi wa 1-0 kwenye fainali za Kombe la Dunia za 1998 nchini Ufaransa kabla ya kuambulia sare tasa kwenye fainali za 2006 nchini Ujerumani.

Dalic anatarajiwa kudumisha mfumo wa 4-3-3 utakaoshuhudia kigogo Luka Modric akiongoza safu ya kati naye mfumaji Ivan Perisic akiwa tegemeo la safu ya mbele.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Bangi yanaswa ikisafirishwa kwa basi la Dreamline

Mary Wambui Mungai kujua hatma yake Januari 10, 2023

T L