Crystal Palace waduwaza Man-City kwenye EPL

Crystal Palace waduwaza Man-City kwenye EPL

Na MASHIRIKA

WILFRIED Zaha aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufungia Crystal Palace mabao 50 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kuongoza waajiri wake kuduwaza mabingwa watetezi Manchester City kwa kichapo cha 2-0 mnamo Jumamosi ugani Etihad.

Zaha alifungulia Palace ukurasa wa mabao katika dakika ya sita baada ya kushirikiana vilivyo na Conor Gallagher aliyezamisha kabisa chombo cha Man-City ya kocha Pep Guardiola katika dakika ya 88. Man-City walikamilisha mchuano huo na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya beki Aymeric Laporte kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza kwa hatia ya kumchezea Zaha visivyo.

Licha ya idadi ya wanasoka wao kupunguzwa, Man-City walisalia imara huku ushirikiano kati ya Gabriel Jesus na Phil Foden ukiwa tishio kubwa kwa Palace ya kocha Patrick Vieira.

Jesus alidhani alikuwa amesawazishia Man-City mwanzoni mwa kipindi cha pili ila bao lake likatupiliwa mbali na refa Lee Mason aliyetumia teknolojia ya VAR kubaini kwamba lilifungwa Foden alipokuwa ameotea.

Guardiola aliyekuwa akisimamia mchuano wake wa 200 katika soka ya EPL alikerwa na hatua ya Palace kuanza kupoteza muda mwanzoni mwa kipindi cha pili na akawa katika mazungumzo ya mara kwa mara na Anthony Taylor aliyekuwa refa msaidizi kwenye mchuano huo.

Mbali na Zaha na Gallagher, wanasoka wengine wa Palace waliojituma zaidi na kumwajibisha vilivyo kipa Ederson Moraes wa Man-City ni Michael Olise, Jordan Ayew na Christian Benteke.

Ushindi wa Palace uliwashuhudia wakikomesha rekodi duni ya kusajili sare katika mechi nne mfululizo ligini. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Man-City kufungwa katika uwanja wao wa nyumbani msimu huu na mara ya nne katika kampeni zote za EPL.

Ingawa Palace waliwahi kushinda Man-City ligini mnamo Disemba 2018 ugani Etihad, ilikuwa mara ya yao ya kwanza kuzamisha miamba hao baada ya majaribio 12 yaliyowazolea alama mbili pekee. Kwa Vieira, ushindi wa Palace ulikuwa spesheli zaidi kwake kwa kuwa aliwahi kuwa mchezaji wa Man-City kabla ya kuwa kocha wa chipukizi kambini mwa kikosi cha wafalme hao.

Bao la Zaha ilikuwa ni mara ya nne kutokana na mechi tano kwa Palace kujiweka kifua mbele katika mechi kabla ya kupoteza kama ilivyokuwa katika mechi tatu za awali. Huku Palace wakijiandaa kuvaana na Wolves katika mchuano ujao wa EPL ugani Selhurst Park mnamo Novemba 6, Man-City watamenyana na Club Bruges ya Ubelgiji kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 3 kabla ya kumenyana na Man-United ligini mnamo Novemba 6, 2021.

You can share this post!

Chelsea wafungua pengo la alama tatu kileleni mwa jedwali...

Juventus washuka hadi nafasi ya tisa kwenye Serie A baada...

T L