Crystal Palace wazamisha chombo cha Brighton na kumweka kocha Graham Stephen Potter ‘pabaya’

Crystal Palace wazamisha chombo cha Brighton na kumweka kocha Graham Stephen Potter ‘pabaya’

Na MASHIRIKA

BEKI Joel Veltman wa Brighton amesema kwamba namna walivyopoteza mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Crystal Palace usiku wa Jumatatu ni kama “wizi wa mabavu” ambao kwa sasa umewasukuma katika “eneo la hatari” jedwalini.

Sogora huyo raia wa Uholanzi alifungia Brighton bao la kusawazisha katika dakika ya 55 baada ya fowadi Jean-Philippe Mateta kuwaweka Palace kifua mbele kunako dakika ya 28.

Licha ya Brighton ya kocha Graham Potter kutamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira iliyowawezesha kuwaelekezea wageni wao makombora 25, Palace walivuniwa alama zote tatu kupitia bao lililofungwa na Christian Benteke katika sekunde ya mwisho.

Matokeo hayo yaliwasaidia Palace kuchupa hadi nafasi ya 13 jedwalini kwa alama 32 sawa na Leeds United. Kwa upande wao, Brighton walishuka hadi nambari 16 kwa pointi 26, nne pekee mbele ya Fulham ambao kwa pamoja na West Bromwich Albion na Sheffield United, wanashikilia nafasi tatu za mwisho.

“Sijaamini kabisa kwamba Palace walishinda mechi hiyo. Ni kama walikuja kwetu kutuvamia na kutuibia alama tatu kwa kutumia mabavu. Tulipata nafasi nyingi za wazi za kuwafunga idadi kubwa ya mabao. Lakini hatukuzitumia vizuri fursa hizo hadi Benteke alipokizamisha chombo chetu,” akasema Veltman.

“Kwa sababu ya matokeo hayo duni dhidi ya Palace, sasa tunakaribia eneo la hatari ambapo itakuwa vigumu zaidi kujitoa. Sasa tuna ulazima wa kusajili ushindi katika mechi ijayo dhidi ya West Brom. Vinginevyo, tutawapa Fulham na Newcastle United motisha ya kutupita,” akaongeza difenda huyo.

Huku Brighton wakitarajiwa kuwa wageni wa West Brom uwanjani The Hawthorns katika mechi yao ijayo ya EPL mnamo Februari 27, Palace watawaalika Fulham uwanjani Selhurst Park mnamo Februari 28, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ronaldo afungia Juventus mawili na kuendeleza masaibu ya...

TANZIA: Mbunge wa Juja afariki