CUE yamtaka Sakaja ajue haifanyi masihara

CUE yamtaka Sakaja ajue haifanyi masihara

NA CHARLES WASONGA

TUME ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) imeshikilia kuwa cheti cha digrii cha Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja kinasalia batili hadi atakapowasilisha stakabadhi zote ambazo tume hiyo ilimwitisha kama ithibati kwamba alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Team nchini Uganda mwaka 2016.

Kwenye taarifa Jumatatu, Juni 20, 2022, mwenyekiti wa tume hiyo Profesa Chacha Nyaigotti pia alikana madai ya Bw Sakaja mwaliko wake kufika mbele yao kuthibitisha uhalali wa shahada yake, haukufanywa kwa njia rasmi.

Mwanasiasa huyo, anayewania kiti cha ugavana wa Nairobi, alisema kuwa alikataa kujiwasilisha kwa afisi za CUE kwa “sababu sikupokea mwaliko rasmi kufanya hivyo.”

“Nilisikia kuhusu habari hizo kupitia magazeti. Sijapokea mwalik rasmi kufika mbele ya CUE kwa hivyo sitaenda huko,” Bw Sakaja akasema kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter.

Lakini katika taarifa yake aliyotuma kwa vyombo vya habari, Profesa Chacha alipouuzilia mbali madai hayo akisema tume yake iliwasilisha barua ya mwaliko kwa Bw Sakaja “kwa njia zote rasmi”.

“Tungependa kujulisha umma kwamba barua yetu ya mwaliko kwa Bw Sakaja iliwasilishwa kwake kwa njia rasmi kupitia jumbe za WhatsApp, ujumbe mfupi na barua rasmi ambayo iliwasilishwa katika afisi za Seneti na kupokelewa rasmi kwa kupigwa muhuri,” Profesa Nyaigotti akasema.

Mwenyekiti huyo wa CUE alitoa wito kwa Bw Sakaja kujiwasilisha mbele yao na stakabadhi hitajika kudhibitisha uhalali wa digrii kuhusu Sayansi ya Usimamizi anayodai kupata kutoka Chuo Kikuu cha Team.

“Njia nyingine ambayo anataka kutumia haitatuzuia kutekeleza wajibu wetu kulinga na sharia,” Profesa Nyaigotti akasema akisisitiza kuwa CUE ndio asasi ya kipekee ya kuthibitisha uhalali wa digrii kutoka mataifa ya kigeni.

Miongoni mwa stakabadhi ambazo tume hiyo iliagiza kwamba Bw Sakaja awasilishe ni risiti za malipo ya karo, barua ya usajili kama mwanafunzi miongoni mwa stakabadhi nyingi nyinginezo.

  • Tags

You can share this post!

Babu Owino akana madai kwamba alichochea fujo Jacaranda

Waitaliano wanusia kutawala mashanidano ya Migration Gravel...

T L