Dada 2 matatani kwa kukeketwa

Dada 2 matatani kwa kukeketwa

Na ALEX NJERU

WANAWAKE wawili kutoka kijiji cha Kagongoni, Kaunti ndogo ya Tharaka Kusini, Tharaka Nithi wanaendelea kuuguza majeraha katika hospitali ya Marimanti, baada ya kukeketwa ili kuepuka laana kwa kuhepa tamaduni hiyo ya tangu jadi.

Wawili hao sasa wanakodolewa macho na kufungwa gerezani baada ya kumaliza matibabu yao, huku wakidai kuwa walilazimika kukumbatia tamaduni hiyo baada ya marehemu nyanya yao kuwajia kwenye ndoto, akiwaonya kuwa ndoa zao zitakuwa mashakani na laana itawaandama milele.

Bi Eunice Kanyua, 30 na Lucy Kanoti, ni dada na wamejaaliwa watoto wanne na watatu mtawalia kwenye ndoa zao.

Walidai kuwa kila wanapolala usiku mapepo huwajia na pia wao huwa wagonjwa kwa sababu ya kutokeketwa.

Ukeketaji wa wanawake ni tabia ambayo imeharamishwa kisheria na serikali na anayepatikana na hatia ya kushiriki tabia hiyo yupo katika hatari ya kufungwa miaka saba gerezani.

Ingawa kuketwa kwao kulifaa kuwa siri, mambo yalitumbukia nyongo baada ya wawili hao kulemewa na majeraha kisha kuanza kuvuja damu nyingi kwenye sehemu zao za siri mnamo Jumatatu.

Iliwalazimu wamfahamishe chifu wa eneo hilo ambaye naye aliwafahamisha maafisa wa polisi. Walikamatwa na baba yao, Samuel Nyamu, 56, mama yao, Flora Kathuure, 52 na ngariba aliyewaingiza kwenye ‘utu uzima’ Hellen Gatembi, 67.

Bw Nyamu, Bi Kathuure na Bi Gatembi wanaendelea kuchunguzwa kwa kushiriki tamaduni hiyo haramu, huku wakizuiliwa katika kituo cha polisi cha Marimanti.

Ingawa hivyo, baba yao amewageuka na kudai kuwa hakuhusika na ukeketaji huo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Tharaka Kusini, Bw Kiprop Rutto, watatu hao watafikishwa mahakamani baada ya dada hao wawili kupona majeraha hayo ya kukeketwa.

Dada hao wawili walieleza wanahabari wakiwa hospitalini kuwa, miaka mingi ya nyuma, walimtembelea nyanya yao aliyekuwa akiugua kisha akawaeleza kuwa lazima watahiriwe kabla ya kuolewa.

Ajuza huyo aliwaeleza kuwa wangekumbwa na changamoto ambazo hakuzifichua kwa sababu ukeketaji ni sehemu ya mila yao ya tangu jadi.

Bi Kanyua aliongeza kuwa walimpuuza nyanya yao ila ndoa yao ikaanza kukumbwa na misukosuko baada ya kujaliwa kifungua mimba.

“Aliamrisha kuwa lazima tukeketwe kwa sababu ni tamaduni ya familia yetu ila tukakataa na tukaolewa bila kupitia tamaduni hiyo,” akasema Bi Kanyua.

Baadaye wanadai, nyanya yao alianza kujitokeza kwenye ndoto zao akilalamika kwa nini walikuwa wamempuuza na kuwaamrisha wakeketwe la sivyo waandamwe na mikosi tele.

Baada ya miaka kadhaa ya mikosi na ndoto za kuogopesha, waliamua kukeketwa ili kunusuru ndoa zao na familia zao huku wakiwa na matumaini ya uwepo wa amani licha ya hatari kuwa wangefungwa jela kwa kushiriki tamaduni hiyo.

“Tulijua kuwa ni kinyume cha sheria kuketwa ila msukumo wa amani na usalama wa familia zetu ulitulazimu kushiriki,” akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Wakati ni amana na rasilimali kubwa...

Kipchoge apigwa jeki na INEOS kutimka kwenye marathon...

T L