Makala

Dada, tabasamu ni ndumba kali ya kuvutia machali

Na BENSON MATHEKA August 16th, 2024 2 min read

KUNA mambo unayofaa kufahamu na kutekeleza ili wanaume wavutiwe nawe na uolewe katika umri wa kufurahia maisha ya ndoa.

Kwanza kabisa, wanaume huwa wanapenda vipusa wanaotabasamu.

Hili ni tabasamu linaloanzia kwa macho na kuangaza uso na mashavu yako.

Tabasamu la uhakika la mwanamke ni ndumba kali inayopagawisha wanaume, linamfanya avutie machali.

Dada, jifunze kutabasamu, kukunja uso kunakuharibia raha na kufanya sura yako nzuri ikose mvuto.

Na usiwe mkali, kuwa mnyenyekevu iwapo unataka kupata na kudumisha mwanamume katika uhusiano.

Hii haimaanishi ujiachilie, elewa unacholenga.  Usiwe mtu wa kujishaua na mwenye majitapo na uchunge ulimi wako.

Usiwe mtu wa kujishasha mbele ya machali. Tabaka sio kitu hapa. Wanaume wa tabaka lako wanaweza kukuambaa kwa sababu ya kudharau wale wa matabaka ya chini.

Jifunze kuheshimu watu wa kila tabaka dada na maisha yatakuwa shwari kwako. Kila mwanamume, awe wa tabaka la juu au la chini anapenda kuheshimiwa.

Unyenyekevu wako haumaanishi ukose kujiamini. Kwa hakika, wanaume huwa wanatiwa kichaa na wanawake wanaojiamini.

Wanaojitambua, wanaojua wanachotaka katika maisha, wenye maono, ari na malengo.

Kujua unachohitaji katika ulimwengu huu dada, kunakufanya upange ndoa yako. Kujiamini, dada, kunakufungulia milango ya mahaba.

Usijifunge, wanaume na wanawake hutafutana. Changamka, toka uende kwa hafla za kanisa, semina. Furahia maisha na kukutana na watu.

Unapofanya hivyo, jikwatue, pendeza na utapendwa.

Kuwa mkarimu na vitu vyote isipokuwa mwili wako.

Usifungue mzinga wako kwa kila anayeonyesha nia ya kukuchangamkia. Usibane maoni na msaada wako kwa mwanamume.

Ukarimu wa mwanamke usio wa mwili wake unavutia wanaume. Dada, usiwe mtu wa kulipiza kisasi.

Mahusiano huja na kwenda kabla ya kupata mume wa ndoto yako. Wasamehe waliokutema, msamehe chali aliyekutusi na yule aliyekuvunja moyo ulipoweka matumaini kwake na kumpa moyo wako.

Angalau ulipata funzo. Wasamehe na usonge mbele na maisha.

Ukiendelea kuanika hasira na kisasi chako kwa wanaume waliokucheza shere, wanaume watakuhepa na utakuwa singo maisha yako yote.

Haya yote yanahitaji demu kuwa na akili.

Wanaume hupenda wanawake wenye akili. Elewa kinachotendeka katika mazingira unayoishi, jipende kwanza ikiwa unataka kupendwa.

Ukijipenda hautajiachilia, jikubali ulivyo. Wanaume hupenda wanawake wanaojipenda kwanza na usilaze damu. Wanaume wa kisasa hawapendi mwanamke mzembe