Dadake marehemu Tob Cohen ataka DPP atimuliwe kazini

Dadake marehemu Tob Cohen ataka DPP atimuliwe kazini

NA RICHARD MUNGUTI

DADA yake marehemu Tob Cohen, Gabrielle Hannah Van Straten aliwasilisha ombi la kutimuliwa afisini kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kwa kukataa kumshtaki wakili Philip Murgor kwa madai alighushi wosia wa nduguye kuhusu ugavi wa mali yake, mahakama kuu iliambiwa Jumanne.

Na wakati huo huo Bi Straten alikanusha mbele ya Jaji Mugure Thande, madai kwamba alishirikiana na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) kunasa mawasiliano ya simu za Majaji na Bw Murgor.

Bi Straten aliangua kilio kortini alipoelezwa na Bw Murgor alipagawa na umiliki wa mali ya nduguye ndipo alipanga kumuua ili airidhi.

Alikana alipanga kumtoa uhai nduguye ili atwae mali yake.

Hata hivyo, Gabrielle alikiri alishirikiana na DCI kunasa mawasiliano ya simu ya Jaji Stellah Mutuku, Bw Murgor na majaji wote waliokuwa wanasikiliza kesi yoyote kuhusu nduguye.

Jaji Mutuku ndiye alikuwa anasikiliza kesi ya mauaji inayomkabili Sarah Wairimu Kamotho anayeshtakiwa kwa kupanga mauaji ya Cohen.

Bw Murgor ndiye anayemwakilisha Sarah Wairimu anayeshtakiwa kwa mauaji ya kinyama ya Cohen kati ya Julai 30 na Septemba 13, 2019.

Jaji Thande anayesikiliza kesi ya ugavi wa mali ya Cohen alielezwa na Bw Murgor kwamba, Gabrielle, alipambana na yeyote yule aliyepinga akimiliki mali ya Cohen kulingana na Wosia alioandika na kuacha kwa wakili Chege Kirundi.

“Ukweli ni kwamba umepagawishwa na umiliki wa mali ya nduguyo hata ukaamua kupambana na kila mtu aliyekuzuia ukiitwaa,” Bw Murgor alimwuliza Gabrielle.

“Ni kweli nimekuwa nikipambana kufa kupona na yeyote ambaye amesimama kati yangu na mali ya ndugu yangu,” Gabrielle alimjibu Murgor.

Alisema alichukua hatua hiyo kusudi haki itendeke katika uchunguzi wa mauaji ya nduguye.

Gabrielle alimweleza Jaji Thande kwamba alipinga Sarah akitwaa umiliki wa jumba la kifahari la Cohen lililo na thamani ya Sh500 milioni pamoja na mamilioni ya pesa zilizo katika Benki za humu nchini na Uholanzi.

“Ulipinga Sarah akiachiliwa kwa dhamana na Jaji Mutuku na pia ukapinga akichukua hata chupi zake na nguo zake kutoka jumba la Cohen?” Bw Murgor alimwuliza Gabrielle.

“Ndio nilipinga mshtakiwa akitwaa mali ya ndugu yangu hata nguo zake,” alijibu Gabrielle.

Bw Murgor alimwuliza Gabrielle ikiwa anaweza onyesha mahakama sehemu aliyobadilisha katika Wosia.

Gabrielle alisema hawezi tambua sehemu ya wosia iliyobadilishwa na Murgor.

Bw Murgor aliwasilisha mahakamani Wosia tatu anazodaiwa alitengeneza Cohen 2012, 2018 na 2019.

Katika wosia wa 2012 na 2018 alikuwa amemtambua Sarah Wairimu Kamotho na bintiye kuwa warithi.

Katika Wosia wa 2019 Cohen alikuwa amemtaja Gabrielle kuwa mrithi wa mali yake.

Sarah amepinga Wosia wa 2019 anaodai umeghushiwa kumpokonya mali ya mumewe.

Kulikuwa na makabiliano makali kati ya mawakili Murgor na Danstan Omari anayewakilisha familia ya marehemu Cohen kuhusu kutokamatwa kwake kuhusu kubadilishwa kwa Wosia wa 2019.

Jaji Thande aliamuru DCI awasilishe Wosia asili aliondika Cohen na kuacha kwa wakili Kirundi kuhusu ugavi wa mali yake.

Kesi inaendelea kusikilizwa.

  • Tags

You can share this post!

Maajenti wa kazi Uarabuni kuchunguzwa

Samboja awindwa tena kuhusu cheti cha chuo kikuu baada ya...

T L