Michezo

Dagoretti High yango’a Kisumu Day kiputeni

August 1st, 2019 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

WENYEJI Kisumu Day wamebanduliwa nje ya michuano ya kuwania ubingwa wa soka miongoni mwa shule za sekondari baada ya kulimwa 2-0 na Dagoretti High School, Jumatano.

Kwenye mechi nyingine uwanjani humo, Ebwali Secondary School ambao awali waliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Kisumu Day, waliagana sare 1-1 na Mbooni High; matokeo ambayo huenda yakawafaidi Mbooni High iwapo watapata ushindi dhidi ya Kisumu Day katika mechi ya mwisho kwenye kundi hilo.

Kisumu Day waliingia uwanjani baada ya hapo awali kushindwa na Ebwali wanaotegemea ufadhili kutoka kwa watu wa kujitolea akiwemo Mbunge Maalum, Godfrey Osotsi, ambapo Kisumu walihitaji ushindi wa kuwaongezea matumaini ya kutinga raundi ya pili.

Juhudi za Benson Oluoch kufungia wenyeji bao la mapema katika mechi hiyo iliyochezewa Moi Stadium ziliambulia patupu baada ya kuzimwa na William John, dakika ya tisa.

Kisumu ambao walianza mechi hiyo kwa kishindo walikaribia kupata bao dakika ya 12 lakini kombora la Benson Odhiambo halikulenga wavu.

Huku wakishangiliwa Kisumu Day walipata nafasi nyingine ya kufunga bao lakini Aldrine Otieno akashindwa kufunga hata baada ya kubakia kipa pekee katika eneo la hatari.

Dagoretti walicheza mchezo wa kuumiliki mpira kwa kiasi kikubwa huku wakitafuta nafasi ya kupenya lakini kipindi cha kwanza kikamalizika zikiwa hazijafungana.

Hatimaye juhudi za Dagoretti zilizaa matunda walipopata bao la kwanza dakika ya 55 kutoka na bao la penalti iliyopigwa na Kuleta.

Penalti hiyo ilipeanwa baada ya mshambuliaji James Laurent kuangushwa kwenye eneo la hatari na Vincent Oluoch.

Kikosi hicho kutoka Nairobi kilijipatia bao la pili dakika ya 73 kupitia kwa Ahmed Abdi.

Katika mechi ya leo, Ebwali ambao wanakamata nafsi ya pili kundini wanahitaji sare dhidi ya Dagoretti High na kusonga mbele.