Makala

DAISY: Tuzae watoto tunaoweza kumudu mahitaji yao ya kimsingi

November 27th, 2020 2 min read

Na LUCY DAISY

WATOTO ni baraka na kila mwanadamu hufurahia sana anapopata mtoto.

Hakuna asiyependa kuitwa mama.

Katika jamii ya Kiafrika na hasa hapo awali, wengi walipenda sana kuzaa watoto wengi. Waliozaa watoto wengi walikuwa na sababu zao baadhi wakisema kuwa njia ya kujilinda hasa iwapo wengine wangeaga dunia.

Wengine waliwataja watoto kuwa baraka na wangekuwa msaada mkubwa katika siku za usoni kwa wazazi wao.

Hata hivyo, jinsi siku zinavyosonga, huduma kama vile za kiafya zinaimarika na kwa hivyo si rahisi kwa watu kuaga dunia wakiwa bado ni wachanga. Pia kwa sasa hali ya kiuchumi imekuwa ngumu na mahitaji ya kuwalea watoto kuongezeka.Kwa mfano wazazi hawana budi kuwapeleka watoto shuleni ili wapate masomo.Hivyo basi majukumu ya kuweza kuwalea watoto yameongezeka.

Hali hizi ni miongoni ya masuala ambayo yametoa changamoto kubwa katika masuala ya ulezi katika maisha ya sasa.

Zamani, watoto wengi walikosa kusoma na kusaidiana na wazazi wao katika kilimo ambapo walihitajika kuhakikisha kuwa wana chakula cha kutosha.

Maisha tunayoishi leo, ni sharti kila mtoto aende shule na pia bei ya vyakula imepanda.Hivyo basi si rahisi kulea watoto 10 kama hapo awali.

Lakini, inashangaza kuwa baadhi bado wanazaa watoto wengi licha ya kupitia hali ngumu kimaisha hasa ya kuweza kuhakikishia watoto hao maisha ya hadhi kwa kutimiza mahitaji ya kimsingi.

Hali hii inachangia katika ongezeko la umaskini hasa kwa kina mama nchini.Kwa mfano watoto wanao randaranda na kuombaomba mitaani siku hizi wameongezeka zaidi. Cha kusikitisha ni kuwa watoto hawa wanaomba pamoja na mama zao.

Kwa maoni yangu, ni vyema wanawake wazae watoto kulingana na uwezo wao wa kuwalea ifaavyo.Haina haja kwa anayefinyika kihela kuzaa watoto wengi.Hali ya kiuchumi ni ngumu mno na si rahisi kuwalea watoto wengi.

Pia ukosefu wa malezi bora ama namna za kujikimu ni miongoni mwa sababu zinazoelekeza baadhi ya watoto hao kwa uhalifu.

Kwa hivyo, ni muhimu kwa wanawake na familia kwa jumla zijitahidi kupanga uzazi ili kuhakikisha kuwa watoto wanaozaa wanapata malezi bora na kuishi maisha yanayofaa.

Jamii haina budi kukubali ya kuwa mambo yamebadilika na wanawake hawana budi kutumia njia zilizopo na zilizokubalika za kupanga uzazi ili kuzuia ongezeko la watoto wengi wasioweza kupata mahitaji yao ya kimsingi.