Makala

DAISY: Vijana wasaidie kudhibiti corona nchini kwa kutii kanuni

October 23rd, 2020 2 min read

NA LUCY DAISY

TANGU mwezi wa Machi, ugonjwa wa corona ulipotangazwa kuingia nchini, watu wengi wameathiriwa na wengine hata kuaga dunia.

Kufikia Alhamisi, takribani watu 47,212 nchini walibainika kuathiriwa huku watu 870 wakiaga dunia.

Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kuwa vijana wanapuuza kuweko kwa ugonjwa huu wa corona.

Vijana hawajali wala hawazingatii sheria zilizowekwa ili kujikinga kutokana na gonjwa hili kwa mfano kuvaa barakoa na kutotangamana.

Pindi tu Rais alipolegeza amri ya kutoka nje mpaka saa tano za usiku, vijana ni kana kwamba walifikiria kuwa corona imeisha.Ukweli ni kuwa ugonjwa huu bado uko na unaendelea kuongezeka.

Mijini sasa, vijana wamerejelea mtindo wa kawaida wa kulewa chakari katika vilabu bila kujali wakati. Hawajali, hawavai barakoa na wanasongamana sana.Wanalewa bila kujali na hata kurejea nyumbani baada ya saa tano usiku.

Kwa kweli kijana mmoja tu aliyeathirika na corona anapokuwa katika klabu fulani ni dhahiri kuwa atawaambukiza wote ukiangalia jinsi wanavyojibeba mle ndani.

Vijana hawana budi kuelewa kuwa ugonjwa huu upo na unaangamiza.

Tumewaona wengi tunaowajua wakiathirika. Vijana wanafaa waelewe kuwa wasipokosa kujichunga na ugonjwa huu, basi wanahatarisha maisha yao na hata ya familia zao.Wanaweza kuwa bado ni barobaro na kuweza kupigana na gonjwa hili linapowashika,lakini wanapolisambazia familia zao hasa wazazi basi watawaua bure kwa kutokuwa makini kwao.

Hivyo basi, vijana hawana budi kuwajibika hata wanapojivinjari.Ni vyema wavae barakoa, wakome kutangamana na wafuate kanuni zote zilizowekwa na wizara ya afya ikiwemo muda wa kurudi makwao.

Serikali pia haina budi kuwachukulia hatua kali vijana wanopuuza na kuzivunja sheria zilizowekwa ili kukabiliana na ugonjwa huu wa corona.

Serikali inapokosa kuchukua hatua kali kwa vijana hawa basi inahatarisha maisha ya wengi hapa nchini.

Wenye vilabu pia hawana budi kuzingatia sheria zilizowekwa na serikali ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu wa corona. Pindi tu saa nne inapowadia, ni bora wafunge vilabu na pia wahakikishe kuwa wateja wao wote wametoka humo ndani.

Jamii na wazazi vilevile wawe katika mstari wa mbele kuongea na kuwasihi vijana kuwa ni jukumu la kila mmoja wao kujilinda na kulinda wawapendao.

Vijana na hata wenye vilabu wanapokiuka sheria hizi jamii haina budi kuwaripoti katika vituo vya polisi ili wachukuliwe hatua zinazofaa.Tukifanya hivyo, tutaweza kukabiliana na janga hili kuu la corona vilivyo.