Makala

DAISY: Wanawake waridhike na maumbile, wasijiumbue

October 29th, 2020 2 min read

Na LUCY DAISY

WANAWAKE wa kisasa wa kiafrika hasa wasichana walioko katika umri wa miaka 20 hadi 30, wamekataa kujikubali kimaumbile.

Kwa mfano, hapa nchini Kenya, vipusa wengi wameamua kujichipua na hata wengine kufanyiwa upasuaji kadha wa kadha ili kubadilisha mionekano yao.

Kuna dhana potovu kuwa msichana mrembo anafaa kukaa jinsi fulani. Lakini mambo kama haya yanafaa kupuuzwa na kutupiliwa mbali kabisa.

Kuna dhana potovu kuwa msichana mrembo anafaa awe mweupe, mwenye umbo dogo, na asiwe na tumbo kubwa na pia ae na nywele za kuangula mgongoni.

Isitoshe awe na midomo miekundu na miembamba na macho yenye nyusi refu.

Lakini wengi wa wasichana katika jamii za Kiafrika wamejaaliwa rangi nyeusi, hawana nywele refu na pia wana mili ni wembamba.

Dhana hii imesababisha wasichana wengi nchini Kenya kuamini kuwa ili wawe warembo ni sharti wajichipue, wengine hata hujinyima chakula ili wakonde, huku wale wenye hela wakikimbilia kwenye hospitali ili kufanyiwa upasuaji wa kutoa mafuta mwilini ili wafaulu kupata mwonekano unaowaridhisha.

Haya yote yana gharama kubwa. Kwani kwa wanaotaka nywele refu hulazimika kununua wigi ama zile zinazowapatia sura wanayoisaka.

Isitoshe, huwa wanajipodoa kupindukia ili wawe na macho ya kupendeza,na nyuso zisizo na doa lolote.

Wasichana wa kiafrika ni warembo sana jinsi walivyo.Haina haja kujaribu kuiga mwonekano wa wengine ili wajihisi warembo.

Ni vyema wafahamu kuwa kuwa ni warembo jinsi walivyo na kujifunza kuridhika na nafsi zao.

Wanapojichipua, kumeza madawa na hata kufanyiwa upasuaji ili wabadilishe mwonekano wao, wajue kuwa wanajiletea madhara mengi mno mwilini na huenda wakapata matatizo ya kiafya katika siku za usoni.

Jamii na viongozi wa kidini hawana budi kuwasihi wasichana wetu kujikubali.Kuwahakikishia ya kuwa ni warembo sana jinsi walivyo na wasiwe na shaka kuhusu urembo wao.

Wanaweza kujisaidia kwa kufanya mazoezi badala ya kutumia dawa ambazo zina athari ya kuwadhuru kiafya.

Wazazi pia wanapowalea watoto wao wa kike ,hawana budi kuwahakikishia kuwa ni warembo jinsi walivyo. Wana jukumu la kuwasaidia waweze kujithamini na sio kuhisi kuwa wamepungukiwa jambop kutokana na maumbile yao.

Ushauri huo wa wazazi utawasaidia hata watakapotangamana na wengine wanaohisi ni tofauti au wana rangi bora zaidi, kujithamini jinsi walivyoumbwa na Maulana.