Daktari akana kunyemelea na kubaka mwanafunzi

Daktari akana kunyemelea na kubaka mwanafunzi

Na RICHARD MUNGUTI

DAKTARI aliyeshtakiwa kwa kumnajisi mwanafunzi wa kidato cha nne aliungama kortini “alivurugana na ndugu ya mlalamishi wakiwa matembezi katika msitu wa Karura.”

Dkt Roy Otieno Ogenyo , mwenye umri wa miaka 23, alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bi Martha Mutuku.

Alikana shtaka la kumbaka msichana aliyetambuliwa kwa jina PNK. Vile vile alikana shtaka la kumpapasa sehemu zake nyeti.

Akiomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana wakili Shadrack Wambui alimweleza hakimu, “Mshtakiwa huyu aliye mbele yako ni daktari na leo yuko hapa kizimbani kwa sababu alitofautiana na ndugu yake mlalamishi katika kesi hii.”

Bw Wambui alisema mshtakiwa “hakumnajisi mlalamishi mbali ni fitina tupu.” Wakili huyo aliendelea kusema,“ukweli utakithiri siku ya kusikizwa kwa kesi hii na uwongo utajitenga.”

Lakini wakili wa mlalamishi alisimama na kudai “mshtakiwa alivuruga ripoti ya daktari aliyempima mlalamishi baada ya tukio hilo.”

Bw Wambui aliomba mahakama imwachilie mshtakiwa kwa kiwango cha chini cha dhamana.

“Naomba hii mahakama imwachilie mshtakiwa kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu. Amelelewa na mama. Mama yake mshtakiwa yuko kortini na yuko tayari kumlipia dhamana isiyo ya kiwango cha juu,” Bw Wambui alimsihi hakimu.

Mahakama ilimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh300,000. Kesi itatajwa Januari 18, 2021

You can share this post!

Jubilee pazuri kutwaa ugavana Nairobi

Bara la Afrika lalala huku dunia ikianzisha chanjo ya corona