Dondoo

Daktari akiona kutongoza mchumba wa makanga

March 24th, 2019 1 min read

NA CORNELIUS MUTISYA

MISUUNI, MACHAKOS

Daktari aliyeheshimiwa eneo hili alikiona kilichomtoa kanga manyoya shingoni kwa kumtongoza kipusa mpenzi wa makanga.

Penyenye za mtaa zaarifu kwamba, daktari huyo alifumaniwa na makanga akiandamana na demu huyo kisha akapokezwa kichapo.

Kulingana na mpambe wetu, makanga huyo alikuwa amejishindia demu huyo walipokutana katika hafla moja kijijini hapa na walikuwa katika hatua za mwisho za kufunga pingu za maisha.

“Makanga alikuwa ametumia taratibu zote kumposa mrembo huyo,” asema mdokezi.

Inasemekana, urembo wa demu huyo ulikuwa ukiwazuzua na kuwapumbaza wanaume wengi. Hakuna mwanaume yeyote aliyekosa kumtupia ndoano wakikutana njiani.

Siku ya tukio, demu huyo alipatwa na homa na akaamua kutafuta matibabu katika zahanati ya karibu.

Alipofika kuhudumiwa, daktari aliyekuwa kwa zamu alizuzuliwa na urembo wa kidosho huyo na akaanza kumtupia mistari.

Baada ya kumhudumia, daktari na mwanadada waliandamana hadi soko ya karibu jamaa akijitetea. Ni wakati huo ambapo makanga aliwaona na akachukua hatua.

Aliwafuata nyuma na aliposikia jamaa akirusha misitari ya mapenzi alimparamia tabibu na kumpa kichapo.

“Utatosheka na mke wako aliye nyumbani. Wacha kuwatamani warembo wa wenyewe,” makanga alisema huku akimgonga daktari huyo.

Duru zaarifu kwamba daktari alitoroka alipoona maji yamezidi unga na kutokomea kusikojulikana.

Kipusa alidai hakuwa na nia ya kumuacha mpenzi wake na kumlaumu makinga kwa kutomwamini.

“Mbona unampiga daktari bila sababu yoyote. Kama ni wanaume unafikiri ningekuwa nimekubali wangapi,”  demu aliwaka.

Kwa upande wake, makanga alidai alimsikia tabibu huyo akimtongoza na hangekubali anyang’anywe kibarafu chake.